Dar es Salaam. Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo ambaye ni
Mwenyekiti wa Chama cha UDP, amesema wanamkaribisha mwanachama wa chama
chochote cha siasa nchini kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, kiongozi
huyo alisema chama hicho bado hakijateua mgombea urais, hivyo milango
iko wazi kwa wanasiasa ambao wako tayari kujiunga na chama hicho kwa
lengo la kuwania nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Hiki chama ni cha Watanzania wote, tunatoa rai
kwa mtu yeyote aliye tayari kuwa mwanachama wetu, milango ya kuwania
urais kupitia chama hiki iko wazi,” alisema Cheyo.
Alisema yeye bado hajaamua kuwania nafasi hiyo kwa sasa, bali muda ukifika atasema, huku akidai kuwa kwa sasa ni mapema kutamka.
Wakati huohuo, Cheyo alisema anasikitishwa na
Ukawa kuendelea kuwahamasisha watu wasiipigie kura Katiba
Inayopendekezwa, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwanyima haki wananchi.
“Raia wote wana haki ya kupigakura, kama Ukawa
wanatembea kila kona ya nchi kuwahamasisha wananchi kuacha kuipigia kura
katiba hiyo ni kosa,” alisema Cheyo.
Kiongozi huyo wa UDP alisema Tume ya Uchaguzi
ndiyo yenye majibu ya mashine za BVR zinazotumika sasa kuandikisha
wapigakura kwenye Daftari la Kudumu kama zinafaa au laa.
Alisema anashangazwa na baadhi ya watu, hususan
wanasiasa na wasomi wanaojitokeza na kusema mchakato wa kuandikisha
wapigakura usimamishwe kwa sababu wanazozijua wao.
“Kwa nini tunatoa majibu ambayo Tume inatakiwa
kuyajibu, ikiwa mashine hazitoshi au ni mbovu, basi yenyewe ndiyo
ituambie. Sasa kama kila mtu anasema lake huo siyo ustaarabu mzuri,
tuache Tume ifanye kazi yake,” alisema Cheyo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji
mstaafu Damian Lubuva alisema bado mashine za uandikishaji wa Daftari la
Wapigakura walizoziagiza kutoka nje ya nchi hazijafika na wanatarajia
zitafika ndani ya wiki mbili zijazo.
Alisema kwa sasa Tume inatumia mashine 250 na kazi
ya uandikishaji mkoani Njombe inaendelea, ikikamilika watatangaza
ratiba ya mikoa mingine.
Awali, Rais Jakaya Kikwete alitangaza rasmi kwamba
tarehe ya upigaji kura ya maoni ya wananchi kuamua kuikubali au
kuikataa katiba inayopendekezwa, itafanyika Aprili 30, mwakani huu.

إرسال تعليق