Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema
analindwa na Mungu na ndiyo maana chama hicho kimegundua mpango wa
mlinzi wake kushawishiwa na maofisa usalama wa taifa ili kumwekea sumu
katika chakula au maji.
Mlinzi huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye
alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay juzi, pia
anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM kuiba siri za chama hicho.
Tayari polisi imeanza kuchunguza taarifa hizo na
jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura
aliliambia gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ana haki kama watuhumiwa
wengine wanaofikishwa polisi wakikabiliwa na kesi za jinai na kusisitiza
kuwa; “Tuhuma zinazomkabili ni za kawaida na tunazichunguza.”
Akieleza alivyopokea taarifa hizo Dk Slaa alisema,
“Ninalindwa na Mungu ndivyo ninavyoweza kusema. Chadema sisi huwa
tunaanza na Mungu na kumaliza na Mungu. Ushahidi umewekwa wazi na hili
ni jambo la kweli na limenigusa kwa kiasi kikubwa.”
Alisema baadhi ya mambo yaliyofanywa na mlinzi
wake ameyaona kwa macho na kusisitiza kuwa njama zinazofanywa na
wanaomtumia haziwezi kukiondoa chama hicho katika harakati zake za kila
siku.
“Tupo makini ndiyo maana tumebaini yote. Tunawajua
waliohusika na tupo makini katika kuwafuatilia. Kama Mungu yupo upande
wetu tumuogope nani zaidi,” alisema.
Alisema Chadema ina safari ndefu hivyo ni lazima
wana-Chadema kuvaa viatu ili kujikinga na vumbi na uchafu wa kila aina,
akimaanisha kuwa chama hicho kinakumbana na vikwazo vingi.
Tuhuma dhidi ya mlinzi huyo zilitolewa juzi na
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando kuwa wamebaini nyendo za
mlinzi huyo na kuzifuatilia kwa ukaribu hadi kupata taarifa hizo
alizosema ni ukweli mtupu.
Hili ni tukio la tatu kwa Chadema kudai kuna
mipango ya kumfuatilia Dk Slaa, mara ya kwanza ilikuwa Februari 2009
alipobaini kutegewa vinasa sauti hotelini mkoani Dodoma na mkakati
uliotajwa kuwa wa kuwaua yeye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akieleza jinsi walivyombaini mlinzi huyo, Marando
alisema pamoja na ushahidi wa mawasiliano ya simu, lakini pia mlinzi
huyo alikiri kwa kinywa chake kutumiwa na maofisa hao ambao hakuwataja
majina lakini alisema wako 22.
“Mlinzi alitueleza kwamba alikuwa akipewa fedha
kwa ajili ya kutoa siri za vikao vya chama kupitia simu yake…kwa kuwa
anaruhusiwa kuingia kwenye vikao vya chama hicho kama mlinzi amekuwa
akitegesha simu yake ili kuwapa taarifa watu wa CCM `live’ ili wasikie
kila kinachojadiliwa,” alidai Marando.
Marando aliyewahi kuwa ofisa wa usalama wa taifa na kuongeza kuwa wako mbioni kufikisha suala hilo polisi.

Post a Comment