Walimu wa michezo wanahitajika shule za msingi

Ni kweli michezo ni burudani, ila kutokana na mabadiliko ya mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, michezo ni kipaumbele katika kutoa ajira pana, kukuza biashara na kujenga jamii bora yenye maelewano.
Kwa mfano, nchi za Ulaya na Marekani, pia nchi za Afrika kama Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon, Tunisia, Morocco, Misri, Afrika Kusini na Algeria zinatumia kikamilifu nafasi hii ya michezo kujitangaza kisiasa na kiuchumi na kutengeneza ajira pana kwa raia wa nchi zao.
Katika hali ya kushangaza sisi Watanzania bado hatujaiona fursa hii pana ya ajira, kama tumeiona basi tunaidharau, maana hatuitendei haki hasa katika ngazi ya msingi.
Hii siyo sawa kabisa, hebu tazameni idadi ya walimu wa michezo waliopo katika shule za msingi za serikali na sekondari, tazameni na uwezo wa walimu hao wa kufundisha michezo, pia tazameni vifaa vinavyotumika pamoja na miundombinu iliyopo.
Ni wazi mkitazama mtaona kuna upungufu mkubwa wa walimu weledi wa michezo katika shule za msingi na sekondari, hali inayosababisha watoto wasipende michezo kwenye shule, hivyo walimu hao wachache na wale wasio na weledi kushindwa kuibua vipaji.
Walimu hao wa michezo ambao hawana ueledi wameshindwa kuonyesha umahiri wao wa kuwabadilisha watoto kwa kuwapa mafunzo sahihi ya michezo kwa sababu kazi ya mwalimu siku zote ni kumbadilisha mwanafunzi kwa kumpa mafunzo sahihi.
Sitaweza kumlaumu mwanafunzi kwa kushindwa kuelewa kwa sababu ya kukosa mwalimu mweledi, lakini nitamlaumu mwanafunzi anayeshindwa kuelewa na kubadilika huku akiwa na mwalimu mweledi, pia nitamlaumu mwalimu asiye mweledi kufundisha wanafunzi, na nitailamu serikali kwa kuwa na walimu wachache wa michezo huku wengine wakiwa hawana ueledi wa kutosha.
Walimu wanaofundisha michezo katika shule za msingi wapo wachache, wapo wenye uwezo ila wengi wao wanahitaji kuendelezwa zaidi ili wawe na uwezo wa kutoa mafunzo mazuri kwa wanafunzi wao.
Wanahitajika walimu weledi wa michezo kufundisha michezo katika shule za msingi na sekondari kwa sababu walimu hao wanatakiwa kuwekeza muda wao na kuwa na uwezo wa kuwafundisha elimu ya viungo, nidhamu, saikolojia na mengine mengi.
Kwa mfano, kipindi cha miaka 6-12 ni kipindi kizuri cha kuendeleza kipaji cha mtoto katika soka na kipindi cha miaka 12-18 ni kipindi kizuri cha kusahihisha yale yote ambayo mtoto aliyakosa wakati wa kuendelezwa kwa ujuzi wake na miaka 19 na kuendelea mtoto anakuwa yupo tayari kwa ajili ya kucheza mchezo wa kulipwa au kucheza timu za wakubwa.
Ndiyo maana nahimiza umuhimu wa kuwapo kwa walimu weledi wa kutosha katika ngazi za chini, katika shule za msingi kwa sababu huko ndiyo msingi imara wa mchezaji unatakiwa kujengwa badala ya kusubiri mwanamichezo amekuwa mkubwa ndiyo apewe mafunzo sahihi na mwalimu mweledi.
Tusijidanganye kabisa kupata wanamichezo weledi ambao michezo kwao itakuwa ajira kama huku kwenye shule za msingi hakuna walimu weledi wanaoweza kutoa mafunzo sahihi kwa watoto ambao tunawategemea kuendeleza michezo mbalimbali.

Post a Comment

Previous Post Next Post