Ni kweli michezo ni burudani, ila kutokana na mabadiliko ya
mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, michezo ni kipaumbele katika
kutoa ajira pana, kukuza biashara na kujenga jamii bora yenye maelewano.
Kwa mfano, nchi za Ulaya na Marekani, pia nchi za
Afrika kama Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon, Tunisia, Morocco,
Misri, Afrika Kusini na Algeria zinatumia kikamilifu nafasi hii ya
michezo kujitangaza kisiasa na kiuchumi na kutengeneza ajira pana kwa
raia wa nchi zao.
Katika hali ya kushangaza sisi Watanzania bado
hatujaiona fursa hii pana ya ajira, kama tumeiona basi tunaidharau,
maana hatuitendei haki hasa katika ngazi ya msingi.
Hii siyo sawa kabisa, hebu tazameni idadi ya
walimu wa michezo waliopo katika shule za msingi za serikali na
sekondari, tazameni na uwezo wa walimu hao wa kufundisha michezo, pia
tazameni vifaa vinavyotumika pamoja na miundombinu iliyopo.
Ni wazi mkitazama mtaona kuna upungufu mkubwa wa
walimu weledi wa michezo katika shule za msingi na sekondari, hali
inayosababisha watoto wasipende michezo kwenye shule, hivyo walimu hao
wachache na wale wasio na weledi kushindwa kuibua vipaji.
Walimu hao wa michezo ambao hawana ueledi
wameshindwa kuonyesha umahiri wao wa kuwabadilisha watoto kwa kuwapa
mafunzo sahihi ya michezo kwa sababu kazi ya mwalimu siku zote ni
kumbadilisha mwanafunzi kwa kumpa mafunzo sahihi.
Sitaweza kumlaumu mwanafunzi kwa kushindwa kuelewa
kwa sababu ya kukosa mwalimu mweledi, lakini nitamlaumu mwanafunzi
anayeshindwa kuelewa na kubadilika huku akiwa na mwalimu mweledi, pia
nitamlaumu mwalimu asiye mweledi kufundisha wanafunzi, na nitailamu
serikali kwa kuwa na walimu wachache wa michezo huku wengine wakiwa
hawana ueledi wa kutosha.
Walimu wanaofundisha michezo katika shule za
msingi wapo wachache, wapo wenye uwezo ila wengi wao wanahitaji
kuendelezwa zaidi ili wawe na uwezo wa kutoa mafunzo mazuri kwa
wanafunzi wao.
Wanahitajika walimu weledi wa michezo kufundisha
michezo katika shule za msingi na sekondari kwa sababu walimu hao
wanatakiwa kuwekeza muda wao na kuwa na uwezo wa kuwafundisha elimu ya
viungo, nidhamu, saikolojia na mengine mengi.
Kwa mfano, kipindi cha miaka 6-12 ni kipindi
kizuri cha kuendeleza kipaji cha mtoto katika soka na kipindi cha miaka
12-18 ni kipindi kizuri cha kusahihisha yale yote ambayo mtoto aliyakosa
wakati wa kuendelezwa kwa ujuzi wake na miaka 19 na kuendelea mtoto
anakuwa yupo tayari kwa ajili ya kucheza mchezo wa kulipwa au kucheza
timu za wakubwa.
Ndiyo maana nahimiza umuhimu wa kuwapo kwa walimu
weledi wa kutosha katika ngazi za chini, katika shule za msingi kwa
sababu huko ndiyo msingi imara wa mchezaji unatakiwa kujengwa badala ya
kusubiri mwanamichezo amekuwa mkubwa ndiyo apewe mafunzo sahihi na
mwalimu mweledi.
Tusijidanganye kabisa kupata wanamichezo weledi
ambao michezo kwao itakuwa ajira kama huku kwenye shule za msingi hakuna
walimu weledi wanaoweza kutoa mafunzo sahihi kwa watoto ambao
tunawategemea kuendeleza michezo mbalimbali.
إرسال تعليق