Hii
ni Picha iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii ikidai kuwa
Gwajima kafariki dunia na yuko Mochwari.Taarifa hizi zilimpa
hofu Gwajima na kumfanya Aagize Bastola yake kwa ajili ya
kujihami.
**********
Utata umeibuka kuhusu bastola waliyodaiwa kukamatwa nayo wafuasi wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima baada ya kiongozi huyo kusema anaimiliki kihalali kinyume na maelezo ya polisi.
Utata umeibuka kuhusu bastola waliyodaiwa kukamatwa nayo wafuasi wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima baada ya kiongozi huyo kusema anaimiliki kihalali kinyume na maelezo ya polisi.
Gwajima aliyetolewa kwenye chumba cha uangalizi
maalumu cha Hospitali ya TMJ jana, amelitaka Jeshi la Polisi kurudisha
bastola hiyo, akisema ni mali yake na aliiagiza ipelekwe hospitalini kwa
sababu ya kujilinda.
Akizungumza na waandishi wa habari
hospitalini hapo alipolazwa baada ya kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu
akiwa katika mahojiano na polisi, Gwajima alisema anashangaa kukamatwa
kwa wachungaji wake waliokuwapo kwa ajili ya kumlinda.
Hata
hivyo, katika kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema bunduki hiyo haina umiliki halali
wa Gwajima wala wa wachungaji 15 waliokamatwa lakini baadaye jioni baada
ya maelezo ya Gwajima, alitoa taarifa akisema bastola hiyo ni mali
halali ya askofu huyo. Pia alisema kuhusu risasi 17 za bunduki aina ya
Shortgun, Gwajima anamiliki bunduki ya aina hiyo lakini akasema
uchunguzi kuhusu watu hao 15 unaendelea.
Kauli ya Gwajima
Akizungumza kwa shida akiwa amejishika tumbo, Gwajima alisema
alipopata taarifa za uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki
dunia, aliagiza wachungaji waende hospitalini kwa ajili ya kumlinda,
lakini wakaishia mikononi mwa polisi wakidaiwa kutaka kumtorosha.Kauli ya Gwajima
Alisema
alihofia kuwapo kwa watu wabaya ambao wangeweza kumdhuru halafu
wakasingizia kitendo hicho kufanywa na polisi kwa kuwa alipata tatizo
akiwa mikononi mwao.
“Usiku wasiwasi ulizidi, huku kila
mmoja akiwa hafahamu kwa nini ujumbe wa namna ile unasambazwa kwenye
mitandao, msambazaji ni nani, ana nia gani, nikaamua kuwaagiza waniletee
silaha yangu iliyokuwa kwenye begi ili likitokea lolote niweze
kujilinda,” alisema Gwajima.
Alisema alishangaa
kukamatwa wachungaji wake na kuchukua silaha iliyokuwa ndani ya begi na
hadi jana hakuwa ameulizwa chochote kuhusu umiliki wa silaha hiyo.
“Kabla
sijazungumza na waandishi kueleza ukweli wa kinachodaiwa kuwa nilitaka
kutoroshwa na wachungaji wangu, nilitaka kuzungumza na ZCO (Mkuu wa
Upelelezi Kanda Maalumu), lakini hajaja, kadi ya ile silaha ninayo,”
alisema Gwajima.
Alisema madai kuwa alitaka kutoroka
ilihali polisi alikwenda mwenyewe akitokea Arusha baada ya kusoma katika
vyombo vya habari kuwa anatafutwa.
Alifafanua kuwa
hata alipofika polisi kwa ajili ya mahojiano hakuwa na shaka hata
kidogo, lakini alishangaa kuona anaishiwa nguvu kila baada ya muda na
alipoona kichwa kinamuuma, akawaomba wampeleke hospitali ili mambo
mengine yafuate baadaye, kitu ambacho hakikufanyika kwa wakati.
Wasiwasi kwa polisi
Alisema
alijaribu kuomba apelekwe hospitali mara kadhaa, lakini hakuna
aliyekubaliana naye hadi alipopoteza fahamu na kupelekwa hospitali ya
Polisi Kurasini.
“Hivi hata kama ni chombo cha usalama,
nimepata matatizo nipo mikononi mwao, halafu nikubali kutibiwa katika
hospitali yao, sikulitaka hilo na hata waliposema nikatibiwe Muhimbili
pia sikutaka, ndiyo maana nilikuja hapa, sisemi moja kwa moja kama
Polisi wanahusika lakini kuna vitu vinanitia shaka,” alisema Gwajima.
Alieleza
kuwa anatilia shaka Jeshi la Polisi kutokana na kuwapo vitu vingi
vinavyoashiria wana kitu kingine wanatafuta, kwani jana tulikuwa na hofu
ya kuvamiwa, waliokuja kutuvamia ni wao, sikugombana na Pengo, nilikuwa
namkemea kama kiongozi mwenzangu wa kiroho wao, wameligeuza ni kesi.
“Sijawahi
kulitilia shaka Jeshi la Polisi lakini katika hili napata wasiwasi
mwingi, sina ugomvi na Kardinali Pengo, nampenda, hajanilaumu, wala
kunishtaki, nilikuwa namkemea katika masuala yetu ya mabaraza ya dini na
siyo vinginevyo,” alisema Gwajima.
Gwajima pia
alionyesha wasiwasi wake kwa kile kilichokuwa kinang’ang’aniwa na polisi
kwenda kupekua nyumbani kwake kuwa hakikuwa kitu kizuri.
Kova alipinga
Wakati
Gwajima akisema hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema bastola waliyokutwa nayo wafuasi wa Gwajima
haimilikiwi kihalali.
“Tumegundua kuwa katika wale watu
waliokuwa pale akiwamo Gwajima mwenyewe, (bastola) haikuwa katika
umiliki wao halali, kwa hiyo hapa kuna kesi ya kupatikana na silaha bila
kibali.”
Akizungumzia tuhuma kwamba polisi walimpekua
mke wa Gwajima, Kova alisema hakuna polisi waliofika nyumbani kwake
kufanya upekuzi wowote na kama wakitaka kufanya hivyo watafuata taratibu
maalumu za upekuzi.
Akijibu swali kuhusu mahali
Gwajima alipotakiwa kutoroshewa, Kova alisema uchunguzi huo bado
unaendelea na utakapomalizika wahusika watafikishwa mahakamani.
Pia
alipoulizwa kama Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amemsamehe Gwajima,
kwani polisi imng’ang’anie, Kova alisema; “amesema anamsamehe lakini
haingilii mambo ya sheria.”
Kuhusu sababu za Gwajima
kuzimia wakati akihojiwa, Kova alisema anayepaswa kuulizwa kwa nini
alianguka wakati akihojiwa na polisi ni Gwajima mwenyewe.
“Siri
za mahojiano huwa hazitolewi kabla ya ushahidi mahakamani, sababu ya
kupata shock (mshtuko) atajua mwenyewe, kwa kuwa ukifanyiwa jambo
ukafurahi au ukachukia wewe ndiyo unajua ilikuwaje, chochote
kitakachotokea ukicheka, ukinuna, ukizimia, wewe ndiyo tukuulize
ilikuwaje mpaka ukazimia kwa sababu hisia unazipata wewe,” alisema Kova.
Makonda amtembelea
Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye alikuwa amemwandikia
Gwajima barua akimwita ofisi kwake, jana mchana alimtembelea hospitalini
hapo kwa ajili ya kumjulia hali kiongozi huyo lakini akasisitiza kuwa
nia yake bado ipo palepale.
“Nilimtaka leo aripoti
ofisini kwangu lakini kwa bahati mbaya anaugua na amelazwa. Nitakwenda
kumuona ili nijue hali yake ikoje,” alisema Makonda kabla ya kufunga
safari kwenda hospitali alikolazwa.
Alisema pia atataka
kiongozi huyo wa kiroho amweleze anavyoelewa maana ya uhuru wa kuabudu
unaoelezwa katika Katiba, usajili wa taasisi yake na katiba ya taasisi
hiyo.
“Mimi ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni. Niliagiza polisi wamkamate na baadaye wakimaliza kumhoji aje kwangu pia atahojiwa na jopo la watu 20,” alisema Makonda.
“Mimi ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni. Niliagiza polisi wamkamate na baadaye wakimaliza kumhoji aje kwangu pia atahojiwa na jopo la watu 20,” alisema Makonda.
Post a Comment