Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema
haoni tatizo kwa vyombo vya habari kuandika kashfa zinazoibua mijadala
kwenye jamii kwa kuwa yanasaidia uongozi kujirekebisha, lakini akaonya
kuwa vyombo hivyo vikitumia uhuru wao kuchochea chuki, vurugu na
mifarakano, Serikali haitavumilia.
Rais Kikwete alikuwa akijibu swali kutoka kwa Tido
Mhando wa Azam Media kuwa, anajisikiaje pale vyombo vya habari
vinapoibua kashfa nzito kama za uchotwaji fedha kwenye akaunti ya escrow
na mkataba wa uzalishaji umeme wa Richmond ambazo alisema zilionekana
kutikisa Serikali.
Tido alimuuliza swali hilo wakati wa mahojiano
maalumu kwenye hafla ya uzinduzi wa studio za kituo cha televisheni cha
Azam TV jana.
“Sioni tatizo,” alisema Rais Kikwete kwenye mahojiano hayo.
Alisema hachukizwi na habari hizo na hana tatizo
na vyombo vya habari, kwani kwa namna moja au nyingine zinasaidia
Serikali yake kujiimarisha na kufanya kazi kwa weledi zaidi.
“Ukiandika masuala ya uchochezi, lazima
tutakuchukulia hatua, lakini mkiandika kuikosoa CCM, hilo sina shida
nalo,” alisema Rais Kikwete.
Licha ya kauli hiyo, Rais Kikwete alisisitiza
kuwa, “Tunatakiwa tuwe na uhuru unaozingatia weledi katika utendaji wa
kazi …Serikali haiwezi kuvumilia kuona baadhi ya vyombo vya habari
vinatumia uhuru huo kuchochea chuki, vurugu na mifarakano katika nchi.”
Akiwa katika moja ya studio zilizoanza kurusha
taarifa ya habari ya saa mbili usiku jana, aliendelea kueleza kuwa,
machafuko yaliyowahi kutokea Rwanda yalichochewa na vyombo vya habari
hadi kufikia hatua wananchi wengine wakawa wanaitwa mende.
Uzinduzi ambao ulifuatiwa na uzinduzi wa jiwe la
msingi pamoja na gari la kurusha matangazo moja kwa moja, (Outside
Broadcasting -OB van).
Ilipofuatiwa hotuba yake, Rais Kikwete alitumia
wasaa huo kummwagia sifa, mmiliki na Mwenyekiti wa Kampuni za Azam, Said
Salim Bakhresa kwa uwekezaji wa studio hizo za kisasa.
“Uwekezaji uliofanywa kwa studio hizi za kisasa ni
mkubwa. Hakuna uwekezaji kama huu uliowahi kufanywa katika sekta ya
habari na utangazaji nampongeza sana Said Bakhressa kwa uwekezaji huu,”
alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa, studio hizo zinaongoza kwa ukubwa
Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alisema, uzinduzi wa studio hizo zilizogharimu
Dola 31 milioni za Marekani sawa na Sh55 bilioni za Tanzania, utapanua
wigo wa ajira, utafungua ukurasa mpya katika tasnia hiyo na kwamba
italeta chachu ya ushindani kwa vyombo vya habari vingine nchini na
Afrika.
Post a Comment