JK akana kuyumbishwa na kashfa za ufisadi

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema haoni tatizo kwa vyombo vya habari kuandika kashfa zinazoibua mijadala kwenye jamii kwa kuwa yanasaidia uongozi kujirekebisha, lakini akaonya kuwa vyombo hivyo  vikitumia uhuru wao kuchochea chuki, vurugu na mifarakano, Serikali haitavumilia.
Rais Kikwete alikuwa akijibu swali kutoka kwa Tido Mhando wa Azam Media kuwa, anajisikiaje pale vyombo vya habari vinapoibua kashfa nzito kama za uchotwaji fedha kwenye akaunti ya escrow na mkataba wa uzalishaji umeme wa Richmond ambazo alisema zilionekana kutikisa Serikali.
Tido alimuuliza swali hilo wakati wa mahojiano maalumu kwenye hafla ya uzinduzi wa studio za kituo cha televisheni cha Azam TV jana.
“Sioni tatizo,” alisema Rais Kikwete kwenye mahojiano hayo.
Alisema hachukizwi na habari hizo na hana tatizo na vyombo vya habari, kwani kwa namna moja au nyingine zinasaidia Serikali yake kujiimarisha na kufanya kazi kwa weledi zaidi.
“Ukiandika masuala ya uchochezi, lazima tutakuchukulia hatua, lakini mkiandika kuikosoa CCM, hilo sina shida nalo,” alisema Rais Kikwete.
Licha ya kauli hiyo, Rais Kikwete alisisitiza  kuwa, “Tunatakiwa tuwe na uhuru unaozingatia weledi katika utendaji wa kazi …Serikali haiwezi kuvumilia kuona baadhi ya vyombo vya habari vinatumia uhuru huo kuchochea chuki, vurugu na mifarakano katika nchi.”
Akiwa katika moja ya studio zilizoanza kurusha taarifa ya habari ya saa mbili usiku jana, aliendelea kueleza kuwa, machafuko yaliyowahi kutokea Rwanda yalichochewa na vyombo vya habari hadi kufikia hatua wananchi wengine wakawa wanaitwa mende.
Uzinduzi ambao ulifuatiwa na uzinduzi wa jiwe la msingi pamoja na gari la kurusha matangazo moja kwa moja, (Outside Broadcasting -OB van).
Ilipofuatiwa hotuba yake, Rais Kikwete alitumia wasaa huo kummwagia sifa, mmiliki na Mwenyekiti wa Kampuni za Azam, Said Salim Bakhresa kwa uwekezaji wa studio hizo za kisasa.
“Uwekezaji uliofanywa kwa studio hizi za kisasa ni mkubwa. Hakuna uwekezaji kama huu uliowahi kufanywa katika sekta ya habari na utangazaji nampongeza sana Said Bakhressa kwa uwekezaji huu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa, studio hizo zinaongoza kwa ukubwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alisema, uzinduzi wa studio hizo zilizogharimu Dola 31 milioni za Marekani sawa na Sh55 bilioni za Tanzania, utapanua wigo wa ajira, utafungua ukurasa mpya katika tasnia hiyo na kwamba italeta chachu ya ushindani kwa vyombo vya habari vingine nchini na Afrika.

Post a Comment

أحدث أقدم