Wakati Mbunge wa Bumbuli, January Makamba akitangaza nia ya
kugombea urais mwaka huu, kada wa CCM Abdul Kaniki ametangaza nia ya
kugombea ubunge kwenye jimbo hilo kumrithi.
Hatua ya Kaniki inafungua ukurasa mpya wa upinzani
ndani ya CCM katika jimbo hilo ambalo mwaka 2010, lilikuwa na wagombea
wanane, akiwamo aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Shelukindo
ambaye alishindwa katika kura za maoni.
Kaniki alikuwa miongoni mwa makada hao waliochuana
vikali kumrithi Shelukindo, kabla ya Makamba kushinda nafasi hiyo bila
kupingwa na upinzani.
“Bado kiu yangu ya kuleta maendeleo katika jimbo
hilo maarufu kwa kilimo cha chai na matunda haijafa. Hivyo, nitarudi
tena kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwaka huu kumrithi Makamba,”
alisema.
Kaniki anataja agenda yake kuu kama atashinda
ubunge kuwa ni kushirikisha wananchi katika kuleta maendeleo katika
nyanja mbalimbali, ikiwamo kilimo, maji, umeme, barabara, elimu na afya.
Katika kilimo, kada huyo (38) anaonyesha
kusikitishwa kwa sekta hiyo kudidimia, hasa baada ya Kiwanda cha Chai
Mponde kufungwa na baadhi ya wakulima kukata tamaa.
“Nikipewa dhamana, kitu cha kwanza ni kuimarisha
mtandao wa kukifanya kilimo chenye tija. Unapozalisha ni lazima
uhakikishe kuna watumiaji,” alisema.
“Kiwanda kikifunguliwa kitaleta ari zaidi kwani
mkulima akiuza chai yake atakuwa ana uwezo wa kununua unga, kulipia
gharama za elimu, kufanya biashara zake na hatimaye kuboresha maisha
yake kwa ujumla.”
Alisema wakulima wa chai katika Jimbo la Bumbuli
walisusa kuzalisha zao hilo wakishinikiza serikali itatue mgogoro wao
kwanza wa kunyanyaswa na kupatiwa ujira ndogo.
Kaniki, ambaye ni msomi mwenye Shahada ya Sayansi
ya Uhandisi wa Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
alisema kuwa kuna kazi nzito ya kuwavutia wakulima waliokata tamaa
warudi kuendelea na kilimo. “Hii ni kazi kubwa inayohusiana na
saikolojia. Wakivutiwa kurudi tutawahamisisha walime pia mahindi na
matunda kwa kuwa Bumbuli ina sehemu kubwa ya maji yanayotiririka na
kustawisha mazao mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa Makamba kashindwa
kufanya hilo kikamilifu.
Kwa mujibu wa Kaniki, uhamasishaji huo utaenda
sambamba na kuhakikisha vijana wanaohitimu darasa la saba na kidato cha
nne wanaacha kuendesha bodaboda na kuingia kwenye kilimo.
Anabainisha kuwa kama mwanasiasa kijana,
mzawa wa Bumbuli anaongozwa na “dhamira, ari na ubunifu katika
ushirikishaji wananchi” ambavyo vitasaidia pia katika kukusanya mapato
mbambali ya kuendeleza miradi ya jimbo.

إرسال تعليق