LIGI YA MABINGWA:Vita ya Messi, Ronaldo yanoga

London, England. Wiki iliyopita zilifahamika timu nane ambazo zimeingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2014/15.
Timu hizo nane ni Real Madrid, Bayern Munich, Paris Saint-Germain, Porto, Barcelona, Atletico Madrid, Monaco na Juventus.
Tayari ratiba ya mechi za robo fainali imepangwa huku mechi za kwanza za hatua hii zikipangwa kuchezwa Aprili 14 na 15 wakati mechi za marudiano zitachezwa Aprili 21 na 22, 2015.
Ratiba hiyo inaonyesha Paris Saint-Germain itakipiga na Barcelona huku Atletico Madrid ikikipiga na Real Madrid wakati Porto itakuwa na kibarua kigumu kwa Bayern Munich, pia Juventus itakipiga na Monaco.
Mpaka sasa katika mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mshambuliaji wa Shakhtar Donetsk, Luiz Adriano ambaye timu yake ilitolewa katika hatua ya 16 bora ya mashindano hayo ndiye anayeoongoza chati ya ufungaji akiwa na mabao tisa akifuatiwa na Lionel Messi (Barcelona) na Cristiano Ronaldo (Real Madrid) ambao wana mabao nane kila mmoja.
Messi na Ronaldo ambao wanakipiga katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), timu zao bado zipo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa hivyo mmojawapo anapewa nafasi kubwa ya kuwa mfungaji bora katika mashindano hayo.
Nyota hawa wamekuwa wakishindana katika kuwania tuzo ya mchezaji bora wa dunia (Ballon d’Or) huku Messi akiitwaa mara nne na Ronaldo mara tatu, pia wamekuwa wakishindana katika kuwania tuzo ya mfungaji bora wa La Liga (Tuzo ya Pichichi).
Hivi sasa Ligi ya La Liga inaendelea huku Messi akiwa anaongoza kwa kufunga mabao akiwa nayo 32 akifuatiwa na Ronaldo mwenye mabao 31.
Pia, Ronaldo na Messi wameishavunja rekodi ya kufunga mabao 50 kwa msimu na kila mmoja ameishafunga zaidi ya mabao 400 katika mechi walizochezea klabu zao na timu za taifa.
Kutokana na rekodi walizonazo,je, ni Messi au Ronaldo atakayeibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi ya mabingwa Ulaya? au watakuwa Karim Benzema (Real Madrid), Carlos Tevez (Juventus) na Edinson Cavani (Paris Saint-Germain) wenye mabao 6 katika mechi za ligi hiyo?
Vita ya Messi, Ronaldo yanoga

Post a Comment

Previous Post Next Post