LULU: NIHURUMIENI JAMANI, Mama yake Ashangazwa na Mambo yanayotokea, ateta na __

Na Sifael Paul
Moyo unauma! Kufuatia kifo cha ghafla cha Kapteni Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Mbunge wa Mbinga Magharibi mkoani Ruvuma kwa ‘leseni’ ya Chama cha Mapinduzi (CCM), John Damiano Mtokambali Komba (61), staa wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anadaiwa kuathirika kisaikolojia kutokana na kushambuliwa mitandaoni.

Staa katika tasnia ya filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
SALAMU ZAANZA
Baada ya Komba kufariki dunia Jumamosi iliyopita, baadhi ya Watanzania wasio na soni walianza kumtumia salamu za pole Lulu kwa madai kwamba aliwahi kutuhumiwa kutoka na mheshimiwa huyo ambaye pia alikuwa mwimbaji mwenye jina kubwa Bongo.

Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Mbinga Mhashamu John Ndimbo akiongoza ibada ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damiano Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma.
Habari kutoka kwa chanzo chetu ambacho ni mtu wa karibu wa Lulu, staa huyo alijikuta akiumia moyo kama walivyo binadamu wengine lakini hali hiyo imekuwa ikimtesa hasa aina ya meseji zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mwanaume ‘akiwa karibu naye’ basi ajiandae kuaga dunia.

MANENO YA KUCHOMA MOYO
“Eti mwanaume kama ana jina linaloishia na ‘mba’ kama Komba au Kanumba (marehemu steven Kanumba) basi imekula kwake,” kilisema chanzo hicho na kufafanua kwamba maneno hayo yameuchoma moyo wa Lulu kiasi kwamba anahitaji ushauri wa kisaikolojia.
Ilisemekana kwamba, hali hiyo imemkosesha raha Lulu na kuwaona baadhi ya Watanzania kuwa ni watu wasiojua maumivu ya moyo kwani naye ana moyo wa nyama na siyo chuma.
Chanzo hicho kilieleza kwamba, kwa umri wa Lulu wa miaka 20 amebebeshwa mzigo mzito mno hadi amefikia hatua ya kutamka waziwazi: “Watanzania imetosha, nimewakosea nini? Naombeni nihurumieni jamani!”

ATHARI ZA KIMASOMO
Kwa mujibu wa chanzo hicho, pamoja na kwamba Lulu anafanya vizuri kwenye masomo yake katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kilichopo Magogoni-Posta jijini Dar, kuna kila dalili akashindwa kufunika kama kawaida yake kutokana na msongo.
“Unajua wakati mwingine anaogopa hata kuingia kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp na Instagram kwa sababu huko ndiko kwenye sarakasi na matusi yasiyokuwa na kichwa wala miguu.

ATHARI ZA KISAIKOLOJIA
“Muda mwingi anakuwa hana raha. Anawaza sana. Hata sisi wenyewe inabidi kumlinda asichukue uamuzi wowote mbaya kwa sababu kiukweli hayupo vizuri kisaikolojia kwani hata yeye mwenyewe anakiri ishu hiyo kumuathiri mno kwenye maisha yake,” kilisema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa popote.

LULU YUPO DARASANI
Baada ya kunyetishiwa ukubwa wa ishu hiyo na namna Lulu anavyoteseka, Ijumaa lilimtafuta staa huyo bei mbaya kwa sasa kwenye Bongo Movies ambapo ilishindikana kwa kuwa alikuwa darasani.

MAMA’KE ASHANGAZWA NA YANAYOTOKEA
Gazeti hili lilipomgeukia mama wa mwigizaji huyo, Lucresia Karugila na kumuuliza namna anavyochukulia ishu hiyo ya mwanaye kuhusishwa kwenye suala hilo alieleza jinsi anavyoshangazwa na kusikitishwa na mambo hayo yanayotokea mitandaoni.
“Nashangaa sana watu wanavyomwandama na kumfuatafuata mwanangu.

AKUMBUSHA KIFO CHA KANUMBA
“Ukweli inasikitisha sana tena sana. Sijui mwanangu amewakosea nini! Hata wakati wa kifo cha Kanumba (Aprili 7, 2012), watu walisema mtu wa mwisho ambaye Lulu aliwasiliana naye ni Komba. Polisi walipochunguza walikuta mtu wa mwisho kuwasiliana naye alikuwa ni Jalia (binamu wa Lulu) na siyo Komba.
“Sijui huwa watu wanatoa wapi mambo ya uongo kiasi hicho. Ifike mahali watu waone huruma jamani, wamuhurumie Lulu kwani hajui chochote maskini,” alisema mama Lulu kwa uchungu.

HUYU HAPA LULU
Baadaye alipotafutwa Lulu alifunguka namna ambavyo amesumbuliwa na jambo hilo akiwashangaa Watanzania kuwa huwa wanatoa wapi mambo ya uongo ambayo hayalengi kumjenga kimaendeleo.
“Awali nilikuwa sielewi, nikawa nashangaa napewa pole, nikajiuliza pole za nini?
“Kiukweli Watanzania wanashangaza sana. Wanapenda sana kuzungumza mambo ambayo hawana uhakika nayo.
“Badala wanishauri mambo ya kazi wanaeneza mambo yasiyokuwa na kichwa wala miguu.
“Naombeni Watanzania wajue pia kuwa na mimi ni binadamu wanihurumie,” alisema Lulu anayeonekana kuumizwa na jambo hilo.

MTAALAM WA SAIKOLOJIA
Kwa mujibu wa mtaalam wa masuala ya saikolojia wa gazeti hili, Amrani Kaima, kama hakutakuwa na tahadhari za kumlinda Lulu asiwe kwenye msongo, madhara yake kisaikolojia yanaweza yasionekane haraka hadi hapo baadaye.
“Cha msingi awapuuze. Ni kikundi au watu wachache tu wala asiumize kichwa kuwawazia. Zaidi sana afanye yale yanayomuwekea heshima mbele ya jamii kwa kuwa yeye ni kioo cha jamii,” alisema mtaalam huyo.

YATOKANAYO
Huko nyuma, kabla ya Komba kukutwa na umauti na kuzikwa Jumanne iliyopita kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa, Ruvuma aliwahi kunukuliwa akikanusha kwamba hajawahi kutembea na Lulu na kwamba habari hizo zilikuwa za uzushi tu

Post a Comment

Previous Post Next Post