Kauli ya Mnikulu, Shaban Gurumo, kwamba hata kama
asingepata mgawo wa Sh. milioni 80.8 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya
VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira, angeweza
kutatua shida zake kwa kuwa anamiliki fedha zaidi ya hizo, imeelezwa
kuwa ni ya dharau, kuudhi na pia ni kejeli kwa Watanzania, ambao wengi
wao ni maskini.
Fedha hizo zinadaiwa kuwa ni sehemu ya zaidi ya Sh. bilioni 200
zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT).
Maoni hayo yalitolewa na watu mbalimbali, wakiwamo wasomi, viongozi
wa taasisi za kiraia na wananchi wa kawaida, ambao baadhi walizungumza
na NIPASHE na wengine kupitia mitandao ya kijamii jana.
KIJO-BISIMBA
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Utawala Bora (LHRC), Dk.
Hellen Kijo-Bisimba, alisema kauli kama hizo zimekuwa zikitolewa kwa
sababu wanaozitoa wanaona Watanzania ni watu wasioelewa kitu.
“Wanasema hivyo, kwa sababu wanaona hakuna anayeweza kufanywa chochote,” alisema Dk. Bisimba.
Hata hivyo, alisema Gurumo na watu wengine mfano wake, wanapaswa kuulizwa wanakozitoa fedha hizo wakiwa watumishi wa umma.
DK. BANA
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk.
Benson Bana, alisema kauli za watu kama Gurumo, mbali ya kuwachanganya
wananchi, ni za kuudhi.
Alisema hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, wamekuwa wakitoa kauli
kama hizo bila kuzipima namna zitakavyopokelewa na kutafsiriwa na
wananchi.
“Watu wa kawaida wanaona ni kejeli. Kama unazo fedha nyingi ni
zako. Kauli ya Gurumo haiakisi maadili mema, hasa kwa Watanzania
maskini. Wanapokea kama ni dharau.” alisema Dk. Bana.
Aliongeza: “Sijawahi kusikia kauli kama hii. Watanzania, ambao ni
maskini wanategemea maadili mema kwa viongozi wao, hawaipokei kauli hiyo
vizuri.”
WANANCHI
Mbali na Dk. Bana na Dk. Bisimba, wananchi wengi wa kawaida
wamekuwa wakitoa maoni kupitia mitandao ya kijamii wakishutumu kauli
hiyo ya Gurumo.
“Huu utukufu wa Ikulu uko wapi? Kama marehemu Baba wa Taifa
alivyosema ni biashara gani kubwa inayofanyika pale mpaka kuzalisha
mamilionea?” alihoji mmoja wa wananchi hao.
Aliongeza: “Kuna mzunguko. Leo hii tunaposikia mfanyakazi wa Ikulu
anasema milioni 80 ni cha mtoto tunakuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu
maisha yetu.”
Afisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Tumaini Makene, alisema kupitia kwa watu kama Gurumo, Watanzania kwa
mara nyingine wanapata fursa ya wazi kuendelea kuongeza sababu za
kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
“Kupitia kauli zinazoweza kusadifu matendo yao nuruni au gizani,
wakiwa kwenye ofisi za umma au nje, lakini wakitamba na dhamana zetu,
akina Gurumo wanazidi kuivua nguo CCM na kuongeza kiu ya Watanzania
kuhitimisha kauli ya Mwalimu Nyerere, 'Watanzania wanahitaji
mabadiliko...nje ya CCM',” alisema Makene.
Aliongeza: “Mtumishi wa umma, tena ofisi kuu ya nchi, akiwa mmoja
wa namba one (moja) wa Rais (na familia kuu?), anapata wapi ujasiri wa
kutamka maneno aliyoyatamka Gurumo mbele ya Baraza la Maadili?”
“Mtumishi wa umma, akiwa na dhamana ya kuwahi kuwa mshauri namba
moja wa masuala ya sheria nchini, anapata wapi ujasiri wa kutamka maneno
aliyosema Andrew Chege mbele ya Baraza la Maadili na nje kwa waandishi
wa habari?
“Mtumishi wa umma, ambaye amekuwa na dhamana ya kuiwakilisha nchi
kimataifa na waziri mwandamizi serikalini, anapata wapi ujasiri wa
kusema maneno aliyoyatamka Prof. Anna Tibaijuka mbele ya Baraza la
Maadili na nje mbele ya waandishi wa habari?
“Ukitafakari sana unaweza kujiuliza kama wanaouthubutu kutamka
maneno haya hadharani, je, wanao uwezo wa kutenda yapi wanapokuwa
wamejifungia kwenye kuta nne za ofisi zetu?
Ujasiri huu unabebwa na mambo kadhaa. Mojawapo ni kiburi cha
kifisadi kinachozidi kumea katikati ya 'rutuba' ya culture of impunity
ya hali ya juu ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa ni kama sera ya kimya
kimya, lakini ikisimama kama moja ya nguzo za CCM.”
Makene alisema watu hao wasingeweza kupata ujasiri huo kama
wangelijua mamlaka ya uteuzi wao ni safi na haiwezi kuvumilia uchafu
wanaojaribu kuipaka.
“Kwamba akina Gurumo, kwa kauli zao zinazosadifu matendo yao,
wanawasaidia Watanzania kujua kiwango cha uadilifu na uwezo wa mamlaka
iliyowateua,” alisema Makene.
Aliongeza: “Nani mwingine atakayetuthibitishia kuwa Ikulu imegeuzwa
pango la walanguzi au wapiga 'deals' kama si akina Gurumo na walioko
nyuma au wakubwa zake kwenye jengo letu la ofisi kuu?”
“Kwamba wakati mama ntilie na baba ntilie wanafukuzwa kinyama
barabarani, huku wakinyang'anywa hata kile kidogo wasichokuwa na uhakika
wa kukipata kesho, watawala wanatamba hadharani kuonesha ukwasi
wanaojilimbikizia kwa kutumia ofisi za umma.”
Alisema wakati wafanyabiashara ndogondogo, maarufu kama
“Wamachinga” wakipigwa mabomu na risasi kwa sababu wanajaribu kutumia
upenyo finyu uliopo kujipatia chochote baada ya viongozi kushindwa
kutengeneza fursa za kila mtu kujitafutia maendeleo, watawala wanatamba
mbele ya vipaza sauti kuwa kutumia ofisi za umma kujitajirisha si lolote
wala chochote. “Hawatishiki.”
Makene alisema pia wakati wananchi wanaosota kutafuta mlo wa siku,
wakilipa kodi kila siku, huku wakichangishwa kila aina ya michango na
serikali, waliokalia ofisi za umma 'wanatamba' kuonyesha kuwa mirija
iliyopaswa kuelekezwa kwenye maendeleo ya wananchi, imeelekezwa mifukoni
mwa wachache.
“Tuwashukuru kwa namna wanavyoiwamba CCM ukutani. Asanteni akina
Gurumo kwa kuongeza mori wa wapigakura...kuiondoa CCM madarakani,”
alisema Makene.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Daudi Mchambuzi,
alisema: “Wanatudharau wananchi , lakini pia wanamdharau huyo Kikwete na
chama chake.”
Gurumo alitoa kauli hiyo juzi wakati akijieleza mbele ya Baraza la
Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu malalamiko yaliyowasilishwa dhidi
yake akituhumiwa kukiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Katika malalamiko hayo, pamoja na mambo mengine, Gurumo anatuhumiwa
kupata fadhila za kiuchumi kutoka kwa Rugemalira na kutotamka fedha
hizo.
Yaliwasilishwa na Wakili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, Hassan Mayunga, mbele ya baraza hilo linaloongozwa na Mwenyekiti
wake, Jaji Hamisi Msumi.
Post a Comment