Maafa ya mvua Kahama ushirikina wahusishwa .

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
 Wakati idadi ya watu waliopoteza maisha katika maafa yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha ikiambatana mawe, upepo mkali na kubomoa nyumba za wananchi Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, ikiongezeka kutoka 42 na kufikia 46, baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamelihusisha janga hilo na ushirikina.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Mwakata wilayani Kahama, Salum Mohamed, alimweleza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwa baadhi ya wananchi wamejenga dhana kuwa tukio hilo limetokana na ushirikina.
Hata hivyo, Pinda aliyewasili hapa jana, aliwataka wananchi hao kuachana na dhana hiyo potofu kuwa mvua zilizonyesha na kusababisha maafa hayo, zimetokana na ushirikina.
Mvua hiyo ilinyesha juzi usiku na kuleta maafa katika vijiji vya Mwakata, Nyumbi na Magung’hwa vilivyopo kata ya Isaka wilayani Kahama.
Idadi hiyo imeongezeka kufuatia majeruhi wanne waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kufariki dunia usiku wa kuamkia jana kuongeza idadi  ya waliokufa katika janga hilo kufikia 46.
Waziri Mkuu, alitembelea vijiji vilivyoathirika na kuwapa pole waathirika na kusema serikali itahakikisha waathirika wote wanapewa msaada unaotakiwa na kwamba tayari chakula kimeanza kugawiwa kwa wananchi na mahema ya kutosha yametolewa. Pinda aliagiza waatalam kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka kambi katika kijiji cha Mwakata kilichoathirika kwa ajili ya kufanya tathmini.
Waziri Mkuu alisema kutokana na janga hilo, kuna uwezekano wa kutokea magonjwa ya mlipuko.
Aidha, aliiagiza timu ndogo ya uratibu wa maafa iliyoundwa na Mkoa wa Shinyanga, isimamie vizuri misaada inayotolewa na wasamaria wema ili iwafikie waathirika wote.
MBUNGE WA MSALALA
Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, ambaye alitembelea katika hospitali hiyo jana, alithibitisha kuwa kati ya walioongezeka ni watoto watatu, wakazi wa kijiji cha Mwakata na mazishi yalifanyika jana katika kijiji hicho.
PINDA AWASILI, ATOA TAMKO 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana aliwasili Kahama na kutembelea vijiji vilivyoathirika na kuwapa pole waathirika na kuwataka wananchi waondokane na fikra potofu kuwa tukio limetokana na masuala ya kishirikina.
Alisema serikali itahakikisha waathirika wote wanapewa msaada unaotakiwa na kwamba tayari chakula kimeanza kugawiwa kwa wananchi na mahema ya kutosha yametolewa.
Pinda aliagiza waatalam kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka kambi katika kijiji cha Mwakata kilichoathirika kwa ajili ya kufanya tathmini.
Waziri Mkuu alisema kutokana na janga hilo, kuna uwezekano wa kutokea magonjwa ya mlipuko.
Aidha, aliiagiza timu ndogo ya uratibu wa maafa iliyoundwa na Mkoa wa Shinyanga, isimamie vizuri misaada inayotolewa na wasamaria wema ili iwafikie waathirika wote.
MISAADA KWA WAATHIRIKA
Serikali kupitia Kitengo cha Maafa kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu, imetoa tani 20 za chakula ambapo kati ya kiasi hicho, maharage tani tano, sukari tani 1.3 na mafuta ya kupikia lita 1,126.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka, katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari alisema misaada mingine iliyotolewa kwa waathirika hao ni blanketi 650, ndoo 82 zenye ujazo wa lita 20, ndoo 82 za lita 10 vifaa vya kupikia seti 82 na madumu 82.
Dk.Turuka alisema misaada zaidi inahitajika kwa waathirika kama vile sare za shule, madaftari ya wanafunzi, mavazi ya kike na kiume na chakula.
“Kwa kuzingatia kuwa waathirika hawa wamepoteza mali na fedha katika maafa haya, misaada ya vifaa vya ujenzi inahitajika, utaratibu wa kupokea misaada hiyo kwa walio Dar es Salaam wanaweza kuiwasilisha Idara ya Kuratibu Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu au kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,” alisema.
Dk.Turuka alisema serikali itaendelea kuwasaidia waathirika dhidi ya changamoto zinazoweza kujitokeza hususani za kiafya zinazosababisha na uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira.
WAZIRI JENISTER MHAGAMA
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Muhagama, alielekeza kuwa misaada yote inayotolewa na wadau mbalimbali isipelekwe makao makuu ya wilaya, badala yake ipelekwe katika eneo la maafa.
Kituo kikubwa cha waathirika kimewekwa katika Shule ya Msingi Mwakata ambako waathirika wamehifadhiwa kwa muda katika majengo matatu.
Mbunge wa Msalala, Maige alimuomba Waziri Mkuu kuangalia uwezekano wa kufuta kodi ya majengo ili vifaa vya ujenzi viuzwe kwa bei rahisi kuwawezesha wananchi kujenga nyumba bora.
Nyumba nyingi zilizobomoka katika tukio hilo zimejengwa kwa matofali ya tope, hivyo mvua kubwa zinaponyesha zinabomoka kirahisi. Maige aliomba ahadi ya serikali ya kuwasaidia waathirika wa tukio hilo ifanyiwe kazi haraka.
Wananchi kwa upande wao, waliiomba serikali kuwajengea vyoo zaidi katika kambi waliyohifadhiwa kwa kuwa wanachokitumia sasa ni kimoja tu. Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Mwakata, Salum Mohamed, alisema kutokana na idadi kubwa ya wananchi walioathirika kuendelea kutumia choo kimoja ni hatari kiafya kwa kuwa kunaweza kutokea magonjwa ya mlipuko.
Mohamed aliomba huduma ya umeme irejeshwe kijijini hapo kufuatia nguzo za umeme zilizokuwapo kuharibiwa na mvua.
DC KAHAMA
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, alisema katika tukio hilo kaya zilizoathirika ni 400 zenye idadi ya watu zaidi ya 1,500.
Mpesya alisema majeruhi 52 ambao ni kati ya 98 waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya wilaya hiyo, wameruhisiwa baada ya hali zao kuwa nzuri.
CUF WATOA SALAMU
Wakati huo huo, Chama cha Wananchi (CUF), kimetoa salamu za rambirambi kwa ndugu na jamaa za watu waliopoteza maisha katika tukio hilo.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Shaweji Mketo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema chama hicho kimebaini kuwa madhara makubwa ya mafuriko yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini yanasababishwa na miundombinu ya mikondo ya maji kutozingatiwa kurekebishwa.
Alisema mfano katika Wilaya ya Kahama, imebainika kwamba wakazi walio pembezoni mwa barabara, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kupunguza madhara endapo barabara zingejengwa mitaro yenye uwezo wa kupitisha maji ili kuyaelekeza mahali stahiki na siyo kwenye nyumba za watu.
Mketo alisema CUF inaitaka serikali kupitia upya utaratibu wa  kukabiliana na majanga makubwa ili kuongeza uharaka wa kuyashughulikia. Alisema serikali inapaswa kuhakikisha mazingira yote yanayoweza kuleta madhara ya mafuriko yanaepushwa mapema na mikondo yote ya maji hasa mito, ilindwe na kuangaliwa mara kwa mara kuhakikisha uwezo wake wa kutiririsha maji unaongeza ufanisi wake.
“CUF kinatoa pole kwa wananchi wote wa Kahama, Moshi, Rufiji, Morogoro na Katavi walioathiriwa na mafuriko haya. Pia CUF inatoa salamu za rambirambi kwa wote waliofiwa na ndugu na jamaa zao katika mvua hizi,” alisema Mketo.
Imeandikwa na Daniel Mkate, Dominic Mohab, Ndalike Sonda, Marco Maduhu, Kahama na Thobias Mwanakatwe, Dar.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post