Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita),
Philip Saliboko (pichani), amefuata nyayo za Mbunge wa Bariadi
Magharibi (CCM), Andrew Chenge, baada naye kukimbilia Mahakama Kuu na
hivyo kukwamisha usikilizaji wa malalamiko yaliyowasilishwa katika
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi yake.
Saliboko analalamikiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma katika baraza hilo kupokea mgawo wa zaidi ya Sh. milioni 40.4
kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited,
James Rugemalira, kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Fedha hizo, ambazo Saliboko anatuhumiwa kupokea, zinadaiwa kuwa
sehemu ya zaidi ya Sh. bilioni 200 zilizochotwa kifisadi katika akaunti
ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hatua ya ‘kukimbilia’ Mahakama Kuu, ilichukuliwa baada ya Jaji
Hamisi Msumi, kutupilia mbali pingamizi la awali la kuzuia malalamiko
hayo kusikilizwa na baraza, yaliyowasilishwa na Saliboko kupitia Wakili
wake, Jamhuri Johnson jana.
Jamhuri aliwasilisha pingamizi hilo baada ya Wakili wa Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga, kuwasilisha malalamiko
hayo dhidi ya Saliboko katika baraza hilo na kuzua malumbano ya kisheria
yaliyodumu takriban dakika 30 kati ya mawakili wa pande mbili hizo
pamoja na Jaji Msumi.
Katika pingamizi hilo, Jamhuri alidai baraza halina uwezo wa
kusikiliza malalamiko dhidi ya mteja wake kwa madai kwamba, kuna amri ya
zuio la Mahakama Kuu kwa chombo chochote cha umma kushughulikia suala
lolote linalohusu kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL) pamoja linalohusu akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Jaji Msumi katika uamuzi wake, alitupilia mbali
pingamizi hilo kwa maelezo kwamba, baraza halimo miongoni mwa walengwa
wa amri ya zuio hilo la Mahakama Kuu na kwa hiyo, haliwahusu.
Pia alisema pingamizi hilo linatupwa kwa sababu kitakachofanywa na
baraza katika usikilizaji wa malalamiko dhidi ya Saliboko,
hakitasababisha ripoti ya CAG ya ukaguzi wa muamala uliofanywa katika
akaunti ya Tegeta Escrow usijadiliwe na Bunge.
“Bado tunasimamia hayo. Kwa hiyo, tunakataa (pingamizi la
Saliboko),” alisema Jaji Msumi. Wakili Jamhuri hakukubaliana na uamuzi
huo Jaji Msumi, hivyo akaomba mteja wake aruhusiwe na baraza kwenda
Mahakama Kuu kuomba marejeo ili kupata tafsiri sahihi juu ya amri ya
zuio hilo.
Jaji Msumi alikubaliana na ombi hilo la Wakili Jamhuri na hivyo,
akaamua kusitisha usikilizaji wa malalamiko dhidi ya Saliboko hadi ombi
la marejeo ya amri ya zuio hilo la mlalamikiwa litakapotolewa maamuzi na
Mahakama Kuu.
Hatua hiyo ya Saliboko imechukuliwa wiki moja baada ya Chenge
kuamua kutimkia Mahakama Kuu kukwepa malalamiko dhidi yake kusikilizwa
na baraza hilo baada ya kuibua hoja ya amri ya zuio hilo mahakamani.
Post a Comment