Tutawataja viongozi wapambe wa wagombea, asema Kinana.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kutoa taarifa ya viongozi waliopewa adhabu kutokana na kuwabeba wagombea wanaosaka nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipozungumza na wajumbe wa mkutano maalum wa CCM wa Jimbo la Mpwapa.
“Utakuta Mbunge yupo, lakini kuna watu wanapita kutaka ubunge, muda ukifika kila mwanachama ana haki ya kugombea, ni matumaini yangu kamati ya siasa ya mkoa na wilaya kutakuwa na mjumbe ambaye hana mgombea,” alisema.  
Alisema haiwezekani mtu afanye siasa kwa kutembea na mgombea wake wakati siyo kazi ya mjumbe wa kamati ya siasa.
“Na akija huko kwako kwenye kamati ya siasa na kuomba umfanyie mpango mwambie wewe ni refa, akija mtu kwako mwambie kuna taratibu zikifika tutakusajili kwa sifa zako,” aliongeza.
Aliwataka viongozi kuwa wakali kwa wanachama wanaokiuka maadili ya chama hicho badala ya kuwaonea haya.
“Katika mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa uliofanyika kule Zanzibar hatukutoa taarifa ya watu hao, lakini tunatafuta muda tutaitoa kwamba kuna watu wamepewa adhabu kutokana na kubeba watu, kuna mwenyekiti wa wilaya kule Zanzibar tumemadhibu kwa kumbeba mtu, yaani yeye amekuwa kipofu haoni wengine  anamuona mmoja tu, na wakati huo Mbunge yupo,” alisema.
Kinana alisema makundi kila sehemu yapo, lakini yanatokana na kutotenda haki na pia kutomteua mtu mzuri anayependwa na watu.
Alisema na migogoro mingi inaletwa na watu ambao hawataki fulani awe kiongozi na matokeo yake anawekwa mtu asiyefaa.
Kinana alisema mtu anajitokeza agombea, lakini anakatwa jina na viongozi ambao hawamtaki.
“Kukatakata majina huko kumesababisha kuchaguliwa viongozi wasiofaa ambao ni wezi, walevi na walanguzi, lakini mtu anapewa uongozi tu kutokana na kuwa na jamaa zake ngazi za juu, kwenye wilaya huko watu wanadhulumiwa sana haki zao na sisi huku juu tumenyamaza,” alisema.
 “Wana CCM tuwe wakali, viongozi tuliomahiri kwa watu tuwe wakali tusikubali, viongozi waliochaguliwa kusimamia maendeleo kuwa wapambe,” alisema.
 “Najua mtaniuliza huyu mtu anaondokaje, ipo namna muulizeni Katibu wa wilaya atawaambia, kama mtu anafanya madudu muondoeni mtafute mtu anayefaa,” alisema.
 Alisema: “Siku moja nilifika Gairo nikakuta diwani ni wa CCM, lakini mwenyekiti ni wa Chadema, nikauliza kwanini nikaambiwa majibu yapo hapo mezani kwako.
Nikauliza ilikuwaje mwenyekiti wa mkoa akanijibu kuna mtu pale anakaa na watu anashirikiana nao vizuri na hodari, lakini walimkata jina lake na kumchagua eti mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa ambaye hakai na watu wala kushirikiani nao.”
Alisema kutokana hali hiyo, wananchi waliamua kumchagua mtu mwingine kwa kuwa walitaka mtu mzuri wakapewa mtu mbovu.

Post a Comment

Previous Post Next Post