Khalid Kangezi akitoa ufafanuzi mbele ya wanahabri (hawapo pichani).
…Akiwa na mwanaye Adam Kangezi (kushoto).
. …Akiendelea kutoa ufafanuzi.
Wanahabari wakifuatilia tukio hilo
ALIYEKUWA mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Khalid Ahmada Kangezi amekanusha
taarifa iliyotolewa na viongozi wa chama chicho kwamba alitaka kumuua
bosi wake, Dk. Wilbroad Slaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam, alisema siku ya kifo cha marehemu Kapteni John Komba
alikuwa akitokea nyumbani kwake Mwenge akielekea kazini nyumbani kwa Dk.
Slaa ambapo baada ya kufika getini aliambiwa na mlinzi wa geti hilo
kuwa haruhusiwi kuingia ndani na alipouliza sababu alijibiwa kuwa
taarifa imetoka kwa mke wa Dk. Slaa.
Alipoendelea kuhoji alipewa majibu kwamba
hapaswi kuendelea kumuuliza maswali ndipo aliamua kurudi tena nyumbani
kujipanga kwa siku ambayo ingefuatia huku akiendelea kufanya juhudi za
kumpata Dr. Slaa ili aweze kumuuliza sababu kuu ya kuzuiwa kuingia
ndani.
Siku iliyofuatia ambayo ilikuwa Jumatatu
ambapo Komba alikuwa anatakiwa kuagwa rasmi, alidamka asubuhi na mapema
kuelekea nyumbani kwa Dk. Slaa kwani alijua kuwa naye angetakiwa
kuungana na viongozi wengine kuuaga mwili wa marehemu. Kwa bahati nzuri
alifanikiwa kumkuta nyumbani japokuwa alizuiwa tena kuingia ndani ila
majibu aliyopewa na Slaa ni kuwa aongee na mkewe wamalizane mgogoro wao
na yeye akasema hakutaka kuingilia mgogoro huo.
Kangezi aliongeza kuwa hakutarajia kama
mke wa Slaa angekuwa na mgogoro naye kwani walikuwa wakiitana mtu na
kaka yake kwa vile wanatoka Mkoa wa Kagera.
Kangezi aliendelea kuelezea kuwa hakuamini
kama kweli angeweza kufungiwa nje ya geti la nyumba kutokana na jinsi
alivyokuwa akihangaika katika kuhakikisha ulinzi wa Dk. Slaa kwa nguvu
ya hali ya juu kutokana na masuala ya vyama na ameishi naye kwa muda wa
zaidi ya miaka 14 bila shida wala tuhuma yoyote.
Baada ya kukosa maelewano nyumbani kwa Dk.
Slaa, aliamua kwenda katika ofisi za chama hicho zilizoko Kinondoni kwa
ajili ya kuonana na kiongozi wake ambapo baada ya kufika alidai alizuiwa
na viongozi wa chama hicho tena wakimtaka kuingia katika chumba maalumu
kwa ajili ya kuchukua mahojiano naye ambapo alifanya kama
alivyotakiwa.
Aliwataja viongozi wa chama hicho
aliowakuta humo ambao tayari walimwamuru kuvua nguo zake zote na kubakia
kama alivyozaliwa huku akitishiwa kuuawa. Humo alitakiwa kueleza
mahusianao yake na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Philip Mangula,
na watu wa usalama wa taifa ambapo alisema alisulubiwa kwa muda wa saa
sita na akitakiwa kuandika katika karatasi kukiri kuwa kweli
anawasiliana nao na kutokana na kipigo alichokuwa akikipata, akihofia
kuuawa, aliamua kutii matakwa yao.
Siku hiyohiyo majira ya usiku alipelekwa
katika hoteli iliyoko maeneo ya Sinza–Madukani ambapo alipakizwa katika
gari lililokuwemo mwanasheria wa chama chicho, Mabere Malando, hadi
kwenye hoteli waliyokuwa wamechukua vyumba na kumwingiza ndani ambako
walianza tena kumsulubu hadi akaishiwa nguvu na akitakiwa tena aandike
kuwa alikuwa na mpango wa kumdhuru Dk. Slaa kwa kumpa sumu,
Kutokana na uchovu aliokuwa nao aliamua kukiri kufanya hivyo huku akirekodiwa.
Alimalizia kwa kusema kuwa hajawahi kufanya jambo lolote la kutaka kumdhuru Slaa, na hata kiasi cha fedha kilichotajwa kuingiziwa na watu wa usalama wa taifa si kweli na hawezi kutunza fedha katika simu. Alieleza pia kwamba amefanya mambo mengi kwa Dk. Slaa na hivyo hawezi kumdhuru licha ya kufahamu siri zake nyingi
Alimalizia kwa kusema kuwa hajawahi kufanya jambo lolote la kutaka kumdhuru Slaa, na hata kiasi cha fedha kilichotajwa kuingiziwa na watu wa usalama wa taifa si kweli na hawezi kutunza fedha katika simu. Alieleza pia kwamba amefanya mambo mengi kwa Dk. Slaa na hivyo hawezi kumdhuru licha ya kufahamu siri zake nyingi
Post a Comment