Moto wawaka majimboni

Dar/Mikoani. Wakati ikiwa imesalia siku chache kabla ya kipenga cha kuruhusu wananchi kujitokeza kuwania urais, ubunge na udiwani, moto unawaka kwenye majimbo mbalimbali ambako wabunge wanapigana vikumbo na watu wanaoonekana kutaka kuwarithi.
Vita iliyo wazi ni ile inayohusisha wenyeviti wa vyama vya NCCR-Mageuzi na TLP, James Mbatia na Augustine Mrema ambao wameshatoleana maneno ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, lakini mchuano ni mkali kwenye majimbo mengine, wakiongozwa na mbunge wa CCM, Ester Bulaya ambaye ameeleza dhamira yake ya kutaka Jimbo la Bunda, ambalo linashikiliwa na Waziri wa Chakula na Kilimo, Steven Wassira pamoja Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu ambaye ameonyesha nia ya kwenda Tanga.
Mchuano huo unazidishwa na kitendo cha wabunge walioingia kwenye Bunge la Kumi kwa tiketi ya viti maalumu, ambao sasa wataka kurejea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kwa kuchaguliwa na wananchi.
Wabunge wengi wa viti maalumu wameanza kuonyesha makucha majimboni wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kile kinachoonekana ni kujiweka karibu na wananchi. Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu.
Kwenye baadhi ya majimbo, mchuano ni mkali zaidi kutokana na ukweli kuwa waliokuwa wanayashikilia na ambao baadhi walikuwa wanaonekana mibuyu, kutangaza kutorudi tena kuomba kura kutokana na kuona imetosha au kufikiria kuwania nafasi nyingine.
Muungano wa vyama vya upinzani, Ukawa, pia umeongeza joto hilo kutokana na ukweli kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi, NLD, CUF na Chadema vimepania kusimamisha mgombea mmoja kwenye majimbo mengi.
“Nimetafakari kufuatia maelekezo ya chama changu, nimejipima na nimetazama hali halisi ya maendeleo na kero ya huduma na matatizo, nikaona ni wakati wa kutatua haya,” alisema Abdulaziz Ahmad alipoulizwa kuhusu nia yake ya kuwania ubunge wa Jimbo la Lindi, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Salum Barwany wa CUF.
Mwanachama mwingine wa CCM, Joseph Mhagama, ambaye analitaka Jimbo la Peramiho linaloshikiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema haoni kama mbunge wa sasa anawatumikia wananchi.
“Nalitaka jimbo kwa lengo la kuleta mabadiliko zaidi kwa kuwa mbunge wa sasa siyo mkaaji jimboni,” alisema Mhagama ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la Ruccodia.
Hata hivyo wabunge wanaotaka kuendelea wanajitetea kuwa wamefanya mengi na wanataka kuyaendeleza.
“Ninajiona kwa sasa hakuna mtu zaidi yangu,” alisema mbunge wa sasa wa Same Magharibi, Dk David Mathayo David alipoulizwa kuhusu kinyang’anyiro cha ubunge jiomboni kwake.
“Nimefanya mengi na bado nataka kuendelea kufanya mengi zaidi lakini natimiza haki yangu ya kidemokrasia kwamba wakati ukifika wa kugombea, haki inaniruhusu. Na mwisho tumeyaanza mengi na tunataka tuendeleze hayo tuliyoanzisha.

Post a Comment

Previous Post Next Post