Dar/Mikoani. Wakati ikiwa imesalia siku chache kabla ya kipenga
cha kuruhusu wananchi kujitokeza kuwania urais, ubunge na udiwani, moto
unawaka kwenye majimbo mbalimbali ambako wabunge wanapigana vikumbo na
watu wanaoonekana kutaka kuwarithi.
Vita iliyo wazi ni ile inayohusisha wenyeviti wa
vyama vya NCCR-Mageuzi na TLP, James Mbatia na Augustine Mrema ambao
wameshatoleana maneno ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, lakini
mchuano ni mkali kwenye majimbo mengine, wakiongozwa na mbunge wa CCM,
Ester Bulaya ambaye ameeleza dhamira yake ya kutaka Jimbo la Bunda,
ambalo linashikiliwa na Waziri wa Chakula na Kilimo, Steven Wassira
pamoja Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu ambaye ameonyesha
nia ya kwenda Tanga.
Mchuano huo unazidishwa na kitendo cha wabunge
walioingia kwenye Bunge la Kumi kwa tiketi ya viti maalumu, ambao sasa
wataka kurejea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kwa kuchaguliwa na
wananchi.
Wabunge wengi wa viti maalumu wameanza kuonyesha
makucha majimboni wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kile
kinachoonekana ni kujiweka karibu na wananchi. Wengi wanajishughulisha
na kuchangia masuala ya maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano
mbalimbali ya mpira wa miguu.
Kwenye baadhi ya majimbo, mchuano ni mkali zaidi
kutokana na ukweli kuwa waliokuwa wanayashikilia na ambao baadhi
walikuwa wanaonekana mibuyu, kutangaza kutorudi tena kuomba kura
kutokana na kuona imetosha au kufikiria kuwania nafasi nyingine.
Muungano wa vyama vya upinzani, Ukawa, pia
umeongeza joto hilo kutokana na ukweli kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi, NLD,
CUF na Chadema vimepania kusimamisha mgombea mmoja kwenye majimbo
mengi.
“Nimetafakari kufuatia maelekezo ya chama changu,
nimejipima na nimetazama hali halisi ya maendeleo na kero ya huduma na
matatizo, nikaona ni wakati wa kutatua haya,” alisema Abdulaziz Ahmad
alipoulizwa kuhusu nia yake ya kuwania ubunge wa Jimbo la Lindi, ambalo
kwa sasa linashikiliwa na Salum Barwany wa CUF.
Mwanachama mwingine wa CCM, Joseph Mhagama, ambaye
analitaka Jimbo la Peramiho linaloshikiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema
haoni kama mbunge wa sasa anawatumikia wananchi.
“Nalitaka jimbo kwa lengo la kuleta mabadiliko
zaidi kwa kuwa mbunge wa sasa siyo mkaaji jimboni,” alisema Mhagama
ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la Ruccodia.
Hata hivyo wabunge wanaotaka kuendelea wanajitetea kuwa wamefanya mengi na wanataka kuyaendeleza.
“Ninajiona kwa sasa hakuna mtu zaidi yangu,”
alisema mbunge wa sasa wa Same Magharibi, Dk David Mathayo David
alipoulizwa kuhusu kinyang’anyiro cha ubunge jiomboni kwake.
“Nimefanya mengi na bado nataka kuendelea kufanya
mengi zaidi lakini natimiza haki yangu ya kidemokrasia kwamba wakati
ukifika wa kugombea, haki inaniruhusu. Na mwisho tumeyaanza mengi na
tunataka tuendeleze hayo tuliyoanzisha.
إرسال تعليق