Kagame amfurahia Jakaya Kikwete

Dar es Salaam. Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuhudhuria mkutano wa tisa wa nchi zilizoungana kutekeleza Miradi ya Miundombinu Ukanda wa Kaskazini za Northern Corridor Projects uliofanyika jijini Kigali, Rwanda, akisema ni hatua muhimu katika kufungua utekelezaji wa miradi ya miundombinu katika kanda nyingine za EAC.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema kuwa Rais Kikwete alihudhuria kikao hicho kwa mwaliko wa Rais Kagame na kwamba mkutano huo ulifanyika kwenye Hoteli ya Serena mjini Kigali.
Naye Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kuwa ni jambo la kufurahisha kwamba Rais Kikwete ameweza kuhudhuria mkutano wa jana kwa sababu sasa njia imefunguka kuanza kazi ya utekelezaji wa miradi kwenye Ukanda wa Kati wa Central Corridor unaokatisha katikati ya Tanzania.
Marais Kagame na Kenyatta walikuwa wanazungumza wakati wa hotuba za ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika zaidi ya saa mbili baada ya Rais Kikwete kuwasili Kigali akitokea Dar es Salaam.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Rwanda. Mbali na nchi hizo, Burundi na Sudan Kusini pia zilialikwa kwenye mkutano huo kujadili hatua za utekelezaji wa miradi mbalimbali kulingana na maelekezo yaliyotolewa katika mkutano wa nane uliofanyika Nairobi, Kenya, Desemba 11, mwaka jana Marais hao wawili wamekuwa wakitofautiana katika suala la waasi wa Rwanda baada ya Rais Kikwete kumshauri Kagame kukaa meza moja na waasi wa Rwanda ili kumaliza tofauti zao zinazosababisha maisha ya watu kupotea.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa Rwanda wakati akizungumza katika kikao cha Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mapema mwaka jana mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambao ulikuwa ukijadili suala la amani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Ukanda wa Maziwa Makuu.
Ushauri huo pia uliwagusa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Joseph Kabila (DRC), ambao aliwataka kufanya mazungumzo na waasi wanaopingana na Serikali zao. Akizungumza katika hotuba yake ya kila mwezi Rais Kikwete alisema: “Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa, kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike.
Rwanda imekuwa ikiituhumu Tanzania kuwa inashirikiana na waasi hao na mara kadhaa magazeti ya nchi hiyo yameripoti taarifa kuwa viongozi wa waasi wa nchi hiyo wamekuwa wakija nchini

Post a Comment

أحدث أقدم