Wanafunzi
watano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ni miongoni mwa watu 50
waliokufa katika ajali ya basi la Majinja, lililogongana na lori katika
eneo la Changarawe Mafinga mkoani Iringa.
Baada
ya magari hayo kugongana, kontena lililokuwa limepakiwa katika lori
hilo lilifyatuka na kupiga basi hilo, hali iliyosababisha mauti kwa watu
50 na majeruhi wengi
Makamu
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema waliopoteza
maisha ni wanafunzi watatu wa mwaka wa tatu na wawili wa mwaka wa pili,
wote kutoka kitivo cha Sayansi ya Jamii (BA Education, COHU).
Alitaja
wa mwaka wa tatu kuwa ni Killeo Eric, Sosten Daud na Chiwangu Didimo na
wa mwaka wa pili katika kitivo hicho ni Watson Jeremiah na Mbaule Frank
aliyekuwa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha UDSM cha Elimu
cha Dar es Salaam (DUCE).
Alisema miili ya marehemu hao imeshachukuliwa na familia zao na kusafirishwa kwa ajili ya maziko.
Profesa
Mukandala alitaja waliojeruhiwa kuwa ni Tupate Mosigwa, ambaye yuko
mwaka wa kwanza, ambaye awali alilazwa katika Hospitali ya Wilaya ya
Mafinga na sasa amehamishiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa
matibabu zaidi.
Mwanafunzi
mwingine aliyejeruhiwa ni Rafael Norbert, aliyekuwa mwaka wa kwanza
DUCE, aliyetibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mafinga na kuruhusiwa
kurejea nyumbani kwa matibabu zaidi.
Profesa
Mukandala alisema uongozi wa chuo hicho unatoa pole kwa familia za
wanafunzi hao pamoja na jamii nzima ya UDSM kwa kupoteza wapendwa hao.
Alisema
chuo hicho kitaendelea kuwasiliana na mamlaka za Mkoa wa Iringa
kufahamu kama kuna majeruhi au marehemu wengine kutoka katika jamii
hiyo, na kutaka wanafunzi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu kwa
kuombea familia za wapendwa waliokufa na waliojeruhiwa.
Uongozi
wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), pia
katika taarifa yake iliyotolewa na Waziri Mkuu wake, Gibson George
iliwashukuru wanachuo wote waliokuwa bega kwa bega katika kutambua
wenzao.
Alisema UDSM imepoteza wanachuo wanne na chuo kishiriki cha DUCE, kimepoteza mmoja na kufanya jumla yao kuwa watano.
Kwa
mujibu wa George, utaratibu wa rambirambi unasimamiwa na Serikali ya
Wanafunzi katika ngazi ya Shule Kuu, chini ya usimamizi wa wenyeviti na
wabunge na mratibu ni Massawe Chrisostom ambae ni Mwenyekiti wa Kitivo
kilichopoteza wanafunzi wanne.
Alisema
kwa niaba ya Daruso wanatoa pole kwa msiba huo na kushukuru uongozi wa
chuo kwa kushiriki katika misiba na kuwatuma wawakilishi kutoka chuoni
hapo.
Ajali
hiyo ilihusisha lori aina ya Scania namba T 689 APJ mali ya Cipex
Company, lililokuwa likiendeshwa na Maka Sebastian (26), ambaye amelazwa
katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa akiendelea na matibabu na basi aina
ya Scania namba T438 CED mali ya kampuni ya Majinja lililokuwa
likiendeshwa na Baraka Gabriel (38) aliyekufa papo hapo.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amesema chanzo cha ajali
hiyo ni ubovu wa barabara katika eneo la ajali na mwendo kasi.

إرسال تعليق