Kuna kila dalili kwamba uhamisho wa Waziri Dk.
Harrison Mwakyembe kutoka Wizara ya Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki,
akibadilishana nafasi na Samuel Sitta, ni sehemu ya kumwepusha na kadhia
ya kashfa ya mabehewa feki ambayo hadi sasa imegundulika kuwa ni kashfa
nyingine inayoitafuna Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
Uchunguzi huru umegundua kuwa hatua ambazo zilianza kuchukuliwa na
Sitta katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA), nako TRL zimeanza
kutikisa baada ya kubainika kwamba mabehewa ambayo yaliingizwa nchini
kutoka China na kupokelewa na Dk. Mwakyembe kwa mbwembwe zote kisha
kubainika hayana viwango, wakubwa wa kampuni hiyo walijua hilo, lakini
wakafunika kombe kwa kuwa wakubwa walipeana zabuni kwa njia ya kujuana.
Habari zinasema kamati iliyoundwa na Sitta kuchunguza kashfa ya
uingizaji mabehewa hayo kutoka India, tayari imeibua mambo mazito ambayo
yanaongeza orodha ya kashfa za ulaji na ufujaji wa fedha za umma
uliosimamiwa na baadhi ya viongozi wa serikali wakitumia madaraka yao
vibaya.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka TRL, uingizaji wa mabehewa
hayo ulifanywa na Kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial
Limited ya India kwa kushirikiana na mfanyabiashara mmoja nchini ambaye
kwa miaka mingi amehusika katika kadhia nyingi za kujipatia fedha kwa
mikataba laghai dhidi ya serikali na mashirika yake.
Vyanzo vyetu ndani ya TRL vinasema kuwa kamati iliyoundwa
kuchunguza kashfa hiyo ya ufisadi wa mabilioni ya fedha, inatarajia
kukamilisha taarifa yake ya uchunguzi hivi karibuni na kuikabidhi kwa
Waziri Sitta, lakini tayari imegundua madudu mengi ikiwamo wakubwa
kupokea mabehewa yenye hitilafu wakati wakijua.
Waziri Sitta amesema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia jambo lolote hadi atakapokabidhiwa ripoti ya uchunguzi.
“Suala la mabehewa feki nimelikuta na kuna tume (kamati) iliundwa
kuchunguza na inatarajia kukamilisha ripoti yake hivi karibini, nadhani
kwa sasa tungevuta subira ila niwahakikishie wananchi sitaogopa kuchukua
hatua bila kujali kashfa hiyo inamhusu mtu au kiongozi wa namna gani,”
alisema. Kashfa ya uingizaji wa mabewa feki iligundulika mwishoni mwa
mwaka jana, ikidaiwa kuwa kuna ufisadi mkubwa umefanyika ndani ya TRL
katika utoaji wa zabuni ya ununuzi wa mabehewa mapya.
Baadhi ya mafundi wa TRL wanasema kuwa mabehewa hayo ni mabovu na hayaendani na vipimo vya reli ya kati.
Udhaifu wa mabehewa hayo uligundulika baada ya kufanyiwa
majaribio, kufuatia mengi ya yale mapya 25 aliyopokea Dk. Mwakyembe
kupata ajali katika mazingira ya kutatanisha, huku ikidaiwa kuwa hayana
‘stability’ yakiwa juu ya reli.
“Unajua hata yale ya mizigo mengi yalianguka sana. Sasa ikaonekana
hebu na haya ya abiria yachekiwe vizuri, nakuambia matokeo yake ni
balaa kama yangeachwa kusafirisha abiria. Ingekuwa ni kilio nchi nzima,”
alisema mtaalam mmoja wa masuala ya reli kwa sharti la kutokutajwa jina
gazetini.
Mabehewa hayo tangu yapokelewe takribani miezi tisa sasa, hayajawahi kusafirisha abiria.
Mtaalam huyo aliongeza kuwa kilichofanyika ni uongozi wa TRL
wakishirikiana na wakubwa wizarani kuengua jopo la mafundi wa TRL na
kuingiza mabehewa hayo kwa kuwa tayari wakubwa walikuwa na mtu wao
katika tenda hiyo.
Dk. Mwakyembe alizindua mabehewa mapya 25 ya kubebea kokoto aina ya
‘Ballist Hopper Bogie’ (BHB), kutoka kampuni ya M/S Hindusthan
Engineering and Industrial Limited yenye thamani ya Sh. bilioni 4.316
kwa ajili ya uimarishaji wa Reli ya Kati.
Upokeaji wa mabehewa ya mizigo ulifuatiwa na tukio jingi la
kushuhudia upokeaji wa mabehewa mengine ya abiria Julai 24, mwaka jana
Dk. Mwakyembe akiwa mmoja wa mashuhuda.
Alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana kuhusiana na kashfa
ya mabehewa feki TRL, Mwakyembe alisema: "Hivi sasa niko nje ya nchi...
vyombo vya habari vimesharipoti sana suala hili. Watu tayari
walishachukuliwa hatua, inawezekana wewe (mwandishi) hujui, wenzako
wameandika sana kuhusu suala hili, na watu walishachukuliwa hatua."
Katika hafla ya upokeaji na ushushaji wa mabehewa hayo katika
Bandari ya Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe alisema ununuzi wake ni sehemu
ya utekelezaji wa makakati wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’ (BRN), ambao
umelenga kuhakikisha usafirishaji wa reli unaimarika kwa ajili ya
kuhimili usafirishaji wa abiria na mizigo, hivyo kusaidia utunzaji wa
barabara za lami zinazojengwa kila kona nchini kwa sasa.
Vyanzo vya habari kutoka TRL vinasema kuwa uhamisho wa Dk.
Mwakyembe kutoka Uchukuzi, ni mkakati wa kumwepusha na kadhia yoyote
ambayo inaweza kulipuka wakati wowote kutokana na zabuni hiyo ambayo
inaonekana kama aina nyingine wa wizi wa wazi.
Mbali na Dk. Mwakyembe, menejimenti ya TRL nayo iko kikaangoni tangu Sitta aunde kamati ya kuchunguza kashfa hiyo
إرسال تعليق