Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imemaliza
kuandikisha wapigakura kwenye daftari la kudumu kwa mfumo wa
kielektroniki (BVR), katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani
Njombe katika kata tisa na kuendelea kwa wiki mbili katika kata za
pembezoni za halmashauri hiyo.
Akizungumza na NIPASHE, Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa
Makambako, Vumilia Nyamoga, alisema uandikishaji umemalizika na
umefungwa katika kata tisa na kwamba uandikishaji utaendelea katika kata
za Kitandililo ambako ulianza juzi.
Alisema kata nyingine ambako uandikishaji ulianza jana ni kata ya
Mahongole ambako utaendeshwa kwa wiki moja. Katika kata ya Utengule
uandikishaji utaendeshwa wiki moja baada ya kumalizika kata hizo mbili.
“Kwa mji wa Makambako ulieenda vizuri kwa siku hizi mbili za
nyongeza na tunaweza kusema wamekamilika wananchi wote kwa kuwa kwa siku
ya leo (jana), ambayo ni ya mwisho baada ya kuongezeka kwa siku mbili
watu wamepungua kabisa,” alisema mkurugenzi huyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Makambako, Chesco Mfikwa, alisema
uandikishaji kwa siku hizo mbili wananchi waliendelea kujitokeza na
kuwa siku ya mwisho ya nyongeza wananchi walijitokeza wachache tofauti
na siku ya kwanza ya nyongeza.
Alisema hadi juzi, walikuwa wamewaandikisha wakazi 44,227 wa kata tisa ambazo uandikishaji ulianzia.
Mmoja wa waandikishaji katika kituo kimoja katika kata ya Mjimwema,
alisema kwa siku mbili walizoongezewa kuna wananchi 115 kwa siku ya
kwanza na siku ya pili kufikia saa saba walikuwa na watu 50
waliowaandikishwa na kuwa walikaa katika kituo hicho kwa muda zaidi ya
saa tatu bila kuja mtu kuandikisha.
“Kwa siku ya leo (jana) watu 50 tu wamefika tangu ashubuhi, lakini
kwa siku ya jana watu 115 tuliwaandikisha na watu hawa isingekuwa
kuongezwa muda watu hawa wasinge kuwa wameandikishwa,” alisema ofisa
huyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق