Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
amesema uchaguzi wa Rais ajaye utakuwa na ushindani mkubwa ndani na nje
ya CCM, huku akibainisha kuwa haogopi mtu kati ya wote wanaotajwa kwenye
kinyang’anyiro hicho, bali anawaheshimu.
Lakini mbunge huyo wa Singida Kaskazini amesema
mgombea pekee atakayemwogopa ni yule atakayekuwa anataka kulipiza kisasi
dhidi ya wagombea wengine.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo jana wakati
alipofanya ziara kwenye makao makuu ya Ofisi za Mwananchi Communications
inayozalisha magazeti ya The Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti zilizoko
Tabata Relini kando ya Barabara ya Mandela.
“Sipendi kulizungumzia sana jambo hilo,” alisema
Waziri Nyalandu ambaye huzungumza kwa sauti ya chini na taratibu...
“Kwenye chama chetu (CCM) muda wake bado. Lakini naweza kusema kuwa
mwaka huu ni wa ushindani mkubwa ndani ya CCM na ‘opposition’,”
aliwaambia wahariri wa Mwananchi Communications.
“Mwisho tutakuwa na kambi ya CCM. Kwaya ya CCM
itapambana na kwaya nyingine ambayo ina sauti zote nne kama CCM,”
alisema akimaanisha kuwa upinzani nao utakuwa umekamilika na kusisitiza
muda ukifika atachukua fomu.
Kauli ya Nyalandu imekuja wakati nchi ikijiandaa
kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu utakaoiweka madarakani Serikali ya Awamu ya
Tano, hali ambayo inaipa shida CCM kumpata mrithi wa Rais Jakaya
Kikwete ambaye pia atalazimika kuachia uenyekiti wa chama hicho.
Tayari wanachama wanne wa CCM wameshatangaza nia,
akiwamo Nyalandu. Wengine ni Hamisi Kigwangala, ambaye ni Mbunge wa
Nzega, January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia) na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda.
Hata hivyo, kinyang’anyiro kikubwa kinatarajiwa
kuwa miongoni mwa makada wa muda mrefu wakiongozwa na Edward Lowassa,
ambaye alikuwa Waziri Mkuu na Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa), ambao hawajatangaza nia, lakini wanatumikia
adhabu ya kufungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kwa makosa ya kukiuka taratibu
za chama hicho kwa kuanza kampeni mapema.
Wengine wanaotajwa kwenye mbio hizo ni Mwigulu
Nchemba, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Mbunge wa Songea Mjini, Emmanuel
Nchimbi, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja.
Wakati CCM ikiwa na kazi ya kumpata mgombea wake
wa urais, hali ni ngumu zaidi safari hii nje ya chama hicho kutokana na
vyama vinne vya upinzani kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja kwenye
kila nafasi.
Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vimeunda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na vimesaini makubaliano ya kusimamisha
mgombea mmoja.
Nyalandu, ambaye alitangaza nia yake wakati akiwa
jimboni kwake, alisema mjadala wa kuelekea Uchaguzi Mkuu unatakiwa
ujikite kwenye masuala ya kuiondoa nchi kutoka hapa ilipo na kwenda juu
zaidi
إرسال تعليق