SAKAT LA KUSHUSHA NAULI, WADAU WATAKA ASKARI WOTE WAWE WANALIPA NAULI KAMA RAIA

WAKATI wadau wa usafiri nchini wakipendekeza kushuka kwa nauli za daladala na mabasi yaendayo mikoani, wamiliki wa mabasi wametishia kufuta utaratibu wa kutowatoza nauli askari na kuongeza kuwa, hata nauli pungufu za wanafunzi sasa zitakuwa historia. 

Wadau wamependekeza kupunguzwa kwa nauli za mabasi yaendayo mikoani kwa viwango vya kati ya asilimia 15 na 25 huku wakitaka nauli za daladala zipungue kutoka Sh 400 hadi Sh 300 kwa njia ya umbali wa kilometa 10. 

Hayo yaliibuka jana wakati wa mkutano wa wadau kukusanya maoni kuhusu mapitio ya viwango vya nauli za mabasi ya mikoani na daladala kupungua kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra). 

Katibu Mkuu wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra­ CCC), Oscar Kikoyo alisema sababu ya kutaka nauli kupungua licha ya kushuka kwa bei ya mafuta, pia wamiliki wa mabasi Julai mwaka 2014 walisamehewa ushuru wa forodha kwa asilimia 10 hadi 25 ya mabasi mapya yanayoingizwa nchini. 

Alisema mafuta yanachangia katika uzalishaji wa huduma kwa asilimia 20 hadi 30 na si jambo jipya katika kuomba kushusha nauli, kwani mwaka 2009 nauli ilishuka ambapo kwa nauli za kwenda mikoani wanataka ipungue kwa km moja kuwa Sh 28.05 badala ya sh 36.89. 

Alitoa mfano wa nauli wanazotaka kwa mabasi ya kawaida kuwa Moshi na Arusha (Sh 17,000 badala ya Sh 22,700), Mwanza (Sh 32,369 badala ya Sh 42,000), Mbeya (Sh 23,365) badala ya sh 30,700), Bukoba (Sh 40,756 badala ya Sh 55,000) na Dodoma (Sh 12,678 badala ya Sh 16,700). 

Katika usafiri wa daladala wamesema wanataka iwe Sh 300 kwa kilometa kuwa Sh 31.39 kwa usafiri wa kilometa 10 badala ya Sh 400 na kilometa 15 iwe Sh 450 na maeneo mengine kupungua kwa Sh 100. 

Kikoyo alisema pia wanaandaa ombi kupitia kanuni na sheria kwa wamiliki wanaotoza nauli kinyume inavyotakiwa walipishwe faini ya Sh milioni moja badala ya Sh 200,000 za sasa ili wayaone maumivu ya adhabu hiyo kubwa. 

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Mabasi ya Daladala (Darcoboa), Sabri Mabruk alisema wao wako tayari kupunguza nauli kwa asilimia mbili hata kesho kama walivyofanya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na siyo asilimia 25 wanayotaka. 

Alisema tatizo kubwa katika ukokotoaji wa hesabu ni suala la ujazo wa abiria ambapo mwaka 2012 walipotakiwa kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia suala hilo ambapo Sumatra wanadai ni asilimia 100, lakini ukweli ni asilimia 80. 

“Ni kweli unaweza kuona mabasi yamejaa, lakini wapo wanafunzi wanaolipa nusu nauli (Sh 200) na askari ambao hawalipi kabisa sasa ni vema kuangalia suala hilo, kwani hata nyakati za mchana mabasi huwa yanaota jua tu, hakuna abiria,” alisema Mabruk alisema ni vema kabla ya nauli mpya kutangazwa kuangalia upya, kwani nafuu ya kupungua bei ya mafuta ni Sh 12,000 ambayo inaishia kwa wafanyakazi hata wamiliki hawaipati. 

“Iwapo mtaamua kushusha nauli tutafuta `ofa’ ya serikali ya kubeba askari bure pamoja na kubeba abiria kwa nusu ya nauli inayotakiwa kisheria na hatutaenda kwenye baraza au mahakamani,“ alisema.

Alisisitiza kuwa ikiwa watatakiwa kwenda mahakamani au kwenye baraza watasimamisha magari yao kufanya kazi, kwani hatua hizo zitakuwa kufidia nauli itakayoshushwa.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi ya Nchini (Taboa), Enea Mrutu alisema hawaoni sababu ya msingi kushusha nauli kulingana na mahesabu na mafuta pekee si kigezo cha kushusha au kupanda nauli na kulalamikia masuala hayo kuingiliwa na siasa

Alishangaa kwa nini suala la kushuka mafuta liwe kwa daladala pekee na siyo vyakula, magazeti na mengineyo kushuka bei huku akisisitiza kuwa changamoto kubwa ni suala la ujazo wa abiria linaloleta utata. 

Huku Katibu wa Chama cha Kutetea Abiria, Thomas Haule alisema wanaunga mkono maombi ya Sumatra CCC katika kupunguza nauli, kwani katika punguzo wamiliki hao wanapata faida kubwa huku akiitaka Sumatra pia kuangalia nauli za abiria wanaoshuka katikati ya safari, kwani hazizingatiwi. 

Pia alitaka kuwe na mfumo maalumu katika kuongeza na kupunguza nauli pindi ikitokea suala kama la kushuka au kupanda bei ya mafuta kuliko kupoteza rasilimali kukaa na kujadili kila wakati.

Credits:habarileo

Post a Comment

أحدث أقدم