Serikali
imesema kuwa ina haki ya kuwahamasisha wananchi kuipigia kura ya ndiyo
Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa ndio iliyohusika kuiandaa.
Naibu
Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu alisema hiyo ni sehemu ya kazi
ya serikali, lakini pia ame wataka viongozi wa dini wafanye kazi yao ya
kuhubiri dini na sio kuingilia masuala ya kisiasa.
Mwalimu
aliliambia Bunge kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambao
walibaki kutunga Katiba walionelea kuwa muundo wa serikali tatu ambao
ulipendekezwa na iliyokuwa Tume ya Kutunga Katiba haikupendekezwa na
wananchi walio wengi.
Alisema
wananchi wengi walitoa maoni yao kwenye masuala ya afya, elimu na
kilimo na ndio maana wajumbe wa BMK waliona mfumo wa serikali mbili
uendelee kama ilivyo sasa.
“Kama
mlikuwa mnataka serikali tatu mngebaki ndani ya Bunge la Katiba, lakini
mliondoka na sisi tuliona serikali mbili ndio wananchi wanayotaka,” alisema.
Alikuwa
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ubungo John Mnyika (Chadema)
ambaye katika swali lake alieleza kuwa muundo wa serikali tatu ndio
ulikuwa unaondoa mgogoro wa namna Zanzibar na Bara wanavyoweza kutoa
marais wa muungano kwa zamu.
Mnyika
alisema kwamba lakini kwa bahati mbaya Katiba Inayopendekezwa ina
muundo wa serikali mbili ambao kamwe hauwezi kuondoa kero na malalamiko
hayo ya lini Zanzibar au Tanzania Bara itoe mgombea urais wa muungano.
Mnyika
alihoji inakuwaje Serikali inakuwa na haki ya kuwahamasisha wananchi
waipigie kura ya ndio Katiba Inayopendekezwa ambayo ina kasoro nyingi;
lakini inawazuia viongozi wa dini pamoja na Ukawa kuhamasisha wananchi
wapige kura ya hapana.
Spika
wa Bunge Anne Makinda baada ya Mnyika kuuliza swali hilo aliingilia
kati na kusema kwamba Ukawa hawatambuliki kikatiba na kwa upande wa
viongozi wa dini alisema hawatakiwi kuhubiri siasa kwenye madhabahu ya
kanisani.
Awali
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Jaku Hashim
Ayoub , Mwalimu alisema Serikali haina dhamira ya kufanya marekebisho ya
Katiba kuhusu utaratibu wa kupata viongozi wa nafasi ya urais kwa zamu
kwa kuzingatia pande mbili za muungano kwa sababu suala la uchaguzi wa
rais ni suala la kidemokrasia.
Mwalimu
alisema kwa mujibu wa misingi ya demokrasia wananchi wanayo haki ya
kumchagua mtu yeyote kutoka sehemu yoyote ya Tanzania ambaye amekidhi
vigezo vilivyoainishwa katika ibara ya 39 ya Katiba.
“Hivyo jaribio lolote la kubana wigo huu wa demokrasia itakuwa ni kinyume na misingi ya demokrasia.”
Alisisitiza
kuwa utaratibu wa upatikanaji wa Rais wa Muungano umeainishwa katika
Katiba ya mwaka 1977 na kufafanuliwa na sheria ya uchaguzi toleo la
mwaka 2002.
Alisema
sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Rais wa muungano zimeainishwa katika ibara
ya 39 ya katiba hiyo. Katika swali lake la msingi, Ayoub alisema baada
ya kumalizika kipindi cha Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye alitoka
upande wa Zanzibar ambayo ni sehemu moja ya muungano hakuchaguliwa
kiongozi mwingine katika ngazi hiyo kutoka upande huo.
Alisema
suala hili ni kilio kikubwa kwa Wazanzibari na lina umuhimu wake katika
kuendeleza na kudumisha misingi ya muungano wetu na hasa katika mwaka
huu wa uchaguzi wa Oktoba 2015.
Aliongeza
kuwa hata Katiba ya Muungano haizungumzii suala la kuweka utaratibu wa
kuruhusu pande hizi mbili kupata viongozi kwa zamu. Alihoji ni lini
Serikali itafanya marekebisho katika Katiba ya Muungano ili kuweka
utaratibu wa kupata viongozi kwa zamu.

إرسال تعليق