Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam inakusudia kutunga sheria kadhaa ndogo, ikiwemo ya kudhibiti ombaomba na uendeshaji wa soko la samaki Feri.
Sheria nyingine zinazotarajiwa kutungwa ni pamoja na sheria za zao la ngozi na za mfuko wa elimu.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Halmashauri ya Ilala ambayo
imesainiwa na Mkurugenzi wake, Isaya Mngurumi imesema mabadiliko hayo ni
kwa mujibu wa kifungu cha 89 cha sheria za Serikali za Mitaa Mamlaka za
Miji sura ya 288 ya mwaka 2002.
Aidha,
sambamba na mabadiliko hayo, vilevile halmashauri hiyo inakusudia pia
kufanya marekebisho katika sheria nyingine ndogo ambazo ni sheria ya
usafi wa mazingira, kodi za majengo na matumizi ya barabara.
Halmashauri
hiyo imewataka wananchi pamoja na wadau wote kujitokeza kutoa maoni yao
na mapendekezo kuhusu utungaji wa marekebisho ya sheria hizo
zilizotajwa.
Aidha,
maoni hayo yametakiwa kuwasilishwa kwa njia ya maandishi katika ofisi
za watendaji kata, ofisi ya mkurugenzi idara ya sheria katika ofisi za
Arnautouglo Mnazi Mmoja kabla ya Machi 31, mwaka huu.

Post a Comment