Pamoja na mpango wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
kuliaga Bunge kukwama jana, Chama cha ACT- Tanzania kimetangaza
kukamilisha maandalizi ya kumpokea mwanasiasa huyo kuanzia leo.
Mbunge
huyo alipanga kuliaga bunge na alisema amekwishapata ruksa ya Spika
kuwa angesimama bungeni kuwaaga wabunge na wanachama wa Chadema baada ya
chama hicho kumtimua uanachama wake hivi karibuni, lakini ghafla mpango
huo uliyeyuka kwa kile kilichoelezwa kuwa Spika amemkatalia.
Tangu
kuanzishwa kwa chama hicho mwaka mmoja uliopita, Zitto amekuwa
akihusishwa kukianzisha, hivyo kitendo chake cha kujiunga nacho
kitahitimisha mjadala wa muda mrefu wa mashabiki wake waliokuwa wakihoji
wapi ataelekea baada ya kung’olewa Chadema.
Akizungumza
na mwandishi jana, Katibu Mkuu wa ACT, Samsom Mgamba aliangua kicheko
na bila kuuma maneno alisema: “Hahahaa... tutampokea kuanzia kesho
(leo) na maandalizi yamekamilika.”
Alipotakiwa kueleza
wapi mapokezi hayo yatafanyika alisema: “Hilo mbona liko wazi,
yatafanyikia makoa makuu yetu (yapo Makumbusho, Dar es Salaam) lakini
kwa taarifa zaidi tutawajuza.”
Zitto anaingia ACT ikiwa
ni siku tisa kabla ya chama hicho kufanya uchaguzi wake mkuu, huku
akitajwa kuwa ameandaliwa kushika wadhifa wa mwenyekiti kuendeleza
harakati zake za siasa.
Hivi karibuni, chama hicho
kilimvua uongozi aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi, Lucas Limbu kutokana
na mgogoro uliokuwapo baina ya viongozi na kufanya nafasi hiyo kubaki
wazi.
Tayari washirika wa Zitto waliohusishwa naye
kuandika waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema na baadaye kufukuzwa
uanachama, Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo wametua ndani ya chama
hicho kipya.
Chama hicho ambacho kinaendelea na
uchaguzi katika ngazi ya mikoa kikibakiza Mkoa wa Geita unaofanya
uchaguzi wake kesho. Kitaanza vikao vyake vya kitaifa Machi 27 na
kuhitimisha kwa mkutano mkuu Machi 29.
Akizungumzia
uchaguzi huo, Mwigamba alisema: “Maandalizi yanakwenda vizuri na hakuna
shaka utafanikiwa kwa kiasi kikubwa na tunawaomba Watanzania watuunge
mkono.”
Tangu juzi, Zitto alitarajiwa kuliaga Bunge
lakini hakufanya hivyo kwa kilichoelezwa kuwa aliitwa na Spika wa Bunge,
Anne Makinda na kupewa ushauri kuwa afanye hivyo jana jioni.
Jana
asubuhi mbunge huyo hakuingika katika kikao cha Bunge lakini alionekana
katika viwanja vya Bunge akiwa amevaa shati la drafti na suruali ya
kaki akizungumza na rafiki yake wa karibu, Deo Filikunjombe ambaye ni
mbunge wa Ludewa kupitia CCM.
Katika kipindi cha jioni,
mbunge huyo aliingia katika viwanja vya Bunge saa 11:10 jioni akiwa
amebeba mafaili huku akizungumza na simu na baadaye kutaniana na
waandishi wa habari waliokuwa nje ya ukumbi wa Bunge.
Mbunge
huyo aliyekuwa amevalia shati nyeupe na suruali nyeupe kabla ya kuingia
ndani ya ukumbi wa Bunge alizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya.
Akwama kuliaga Bunge
Habari
zilizopatikana bungeni jana jioni zilieleza kuwa Spika Bunge, Makinda
alimpiga ‘stop’ mbunge huyo kuaga bungeni bila kuweka wazi sababu za
kufanya hivyo.
Mbunge huyo juzi alitinga bungeni kwa
mara ya kwanza tangu Chadema kitangaze kumvua uanachama na kufanya kikao
cha siri na Makinda kwa zaidi ya saa moja na baadaye kulieleza gazeti
hili kuwa angezungumzia hatima ya ubunge wake jana.
Habari
zilizotufikia na kuthibitishwa na watu wake wa karibu naye
zilieleza kuwa licha ya Makinda kumshauri mbunge huyo kuaga bungeni,
jana aligoma kumpa ruhusa hiyo.
“Kazuiwa kuaga sijui
kwa nini, ila kwa jinsi tunavyoona Makinda ni kama anahitaji Zitto
aendelee kubaki bungeni. Ngoja tusubiri kwanza tuone nini kitatokea,”
zilieleza habari hizo.
Alipoulizwa juu ya taarifa hizo
Zitto, alisema: “Hata mimi nasikia hivyo ila sina hakika sana. Ngoja
niende ndani nitajua zaidi, mimi nataka kuaga, can’t stay any more
(siwezi kuendelea kubaki)."
Alipoingia katika ukumbi wa
Bunge, Zitto alionekana akizungumza na baadhi ya wabunge wa upinzani na
baadaye wakati mjadala wa muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya
Uhamiaji ukiendelea, alitoka nje na watu wa karibu wa mbunge huyo
walisema alikuwa akishinikiza kuaga kama alivyopanga.
Spika
Makinda hakupatikana kuzungumzia sababu za kukataa kumruhusu mbunge
huyo na Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipoulizwa juu ya
suala hilo alisema hajui chochote.
Mbunge wa Tabora
Mjini (CCM), Ismail Aden Rage alisema mbunge huyo kisheria hana mamlaka
ya kushinikiza kuaga bungeni na kumtaka asubiri mamlaka husika zifanye
kazi hiyo, akimaanisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kulijulisha Bunge
kuwa Zitto si mbunge tena baada ya kupata barua ya Chadema.
Chadema
ilitangaza kumvua Zitto uanachama siku 10 zilizopita, saa chache baada
ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kutupa shauri lake alilofungua
akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho
kumpa nyaraka za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote.
Awali,
Mahakama hiyo ilitoa amri ya muda ya kuzuia Chadema kumjadili na
amedumu kwenye nafasi ya ubunge chini ya zuio hilo kwa takribani mwaka
mmoja
Post a Comment