Tabora. Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ameitaka Tume ya
Taifa ya Uchaguzi(Nec) kuhakikisha vyama vyote vinapata haki pamoja na
kulindwa na sheria katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Sumaye alisema hayo jana katika harambee ya ujenzi
wa Kanisa la Moravian, Wilaya ya Tabora Mjini.Alisema vyombo vya dola
havina budi kuhakikisha kampeni zinakuwa na utulivu.
Sumaye aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, alizungumzia zaidi suala la udanganyifu katika matokeo na wizi wa kura.
Katika hilo, alisisitiza usimamizi madhubuti na ulinzi katika vituo vya upigaji kura.
“Hili ni eneo nyeti na kama hakuna uwazi wa
kutosha, fujo na umwagaji damu huweza kutokea. Hapa ndipo panapotokea
udanganyifu katika kuhesabu au hata kuibiwa kura moja kwa moja. Tume
iweke usimamizi madhubuti,” alisema.
Sumaye aliwataka kutumia fursa katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu kwa kuepuka kununuliwa na wanasiasa ili wapambane na
dhuluma zilizojaa nchini.
“Watanzania naomba tuamke na tukatae kununuliwa
kama bidhaa za sokoni au za mnadani. Najua fedha ni kishawishi kikubwa
katika hali hii ya umaskini.
“Kama tunataka kupambana na dhuluma zilizojaa
nchini mwetu, pazuri pa kuanzia ni kupambana na rushwa nyakati za
chaguzi zetu,” alisema Sumaye.
Askofu Isaac Nicodemu aliwataka Watanzania kuwa shupavu katika uchaguzi ujao na kumchagua kiongozi mwenye maadili.
Aliwasisitiza waumini kuendeleza mshikamano katika ujenzi wa kanisa hilo na kuhimiza upendo kwa kila mmoja
Post a Comment