Bunda. Utaratibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
wa kutaka mwanachama anayehitaji kugombea nafasi mbalimbali katika
Uchaguzi Mkuu ujao kujigharimia mikutano yote ya kujinadi, umewaweka
njia panda baadhi ya waliotangaza nia wilayani hapa.
Hali hiyo ilidaiwa kujitokeza juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Stendi ya Zamani mjini Bunda.
Ilielezwa kuwa, mkutano huo uligharimiwa na Pius Masururi aliyetangaza nia kugombea ubunge mjini Bunda.
Baadhi ya waliotangaza nia ambao walikuwapo eneo
la mkutano walisema utaratibu huo hauna budi kuachwa kwa kuwa unawanyima
haki maskini na kuwabeba matajiri, jambo ambalo ni hatari kwa chama
hicho.
Hadi sasa wanachama tisa wa Chadema wameshatangaza
nia ya kuwania ubunge mjini Bunda, jimbo ambalo linaloshikiliwa na
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ambaye pia
ametangaza nia ya kulitetea.
Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Bunda, Samuel
Imanani alisema utaratibu huo uliotolewa na chama Makao Makuu, hauna
budi kufuatwa na kila mwanachama mwenye uchungu.
Alisema utaratibu huo ni kipimo cha mwanachama kama anaweza kukihudumia chama.
Katika mkutano huo uliohutubiwa pia na viongozi
mbalimbali wa Chadema, Masururi alitumia takriban dakika 20 kusisitiza
nia yake ya kugombea nafasi hiyo huku akijinadi kujipanga kumng’oa
Wasira.
Masururi alisema kinachomsukuma kugombea nafasi
hiyo ni matokeo ya uwakilishi mbaya uliopo ambao umekwamisha kwa kiwango
kikubwa ukuaji wa maendeleo ya jimbo hilo, lililojaa rasilimali nyingi
huku wakazi wake wakiwa maskini.
Pia, aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili wapate haki ya
kuwachagua viongozi wao.
Mwingine aliyehutubia mkutano huo ambaye pia
ametangaza nia ni Joyce Sokombi, aliyewataka wakazi wa Bunda kubadilika
kifikra kwa kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
Post a Comment