Utaratibu Chadema sasa walalamikiwa

Bunda. Utaratibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wa kutaka mwanachama anayehitaji kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao kujigharimia mikutano yote ya kujinadi, umewaweka njia panda baadhi ya waliotangaza nia wilayani hapa.
Hali hiyo ilidaiwa kujitokeza juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Stendi ya Zamani mjini Bunda.
Ilielezwa kuwa, mkutano huo uligharimiwa na Pius Masururi aliyetangaza nia kugombea ubunge mjini Bunda.
Baadhi ya waliotangaza nia ambao walikuwapo eneo la mkutano walisema utaratibu huo hauna budi kuachwa kwa kuwa unawanyima haki maskini na kuwabeba matajiri, jambo ambalo ni hatari kwa chama hicho.
Hadi sasa wanachama tisa wa Chadema wameshatangaza nia ya kuwania ubunge mjini Bunda, jimbo ambalo linaloshikiliwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ambaye pia ametangaza nia ya kulitetea.
Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Bunda, Samuel Imanani alisema utaratibu huo uliotolewa na chama Makao Makuu, hauna budi kufuatwa na kila mwanachama mwenye uchungu.
Alisema utaratibu huo ni kipimo cha mwanachama kama anaweza kukihudumia chama.
Katika mkutano huo uliohutubiwa pia na viongozi mbalimbali wa Chadema, Masururi alitumia takriban dakika 20 kusisitiza nia yake ya kugombea nafasi hiyo huku akijinadi kujipanga kumng’oa Wasira.
Masururi alisema kinachomsukuma kugombea nafasi hiyo ni matokeo ya uwakilishi mbaya uliopo ambao umekwamisha kwa kiwango kikubwa ukuaji wa maendeleo ya jimbo hilo, lililojaa rasilimali nyingi huku wakazi wake wakiwa maskini.
Pia, aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili wapate haki ya kuwachagua viongozi wao.
Mwingine aliyehutubia mkutano huo ambaye pia ametangaza nia ni Joyce Sokombi, aliyewataka wakazi wa Bunda kubadilika kifikra kwa kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Post a Comment

أحدث أقدم