Koba: Dakika tisa ulingoni zilinipa kazi

Koba Kimanga ni miongoni mwa mabondia waliotamba na timu ya Taifa ya ngumi kati ya mwaka 1978 hadi 1998.
Koba kwenye ndondi
“Nilianza kucheza ngumi nikiwa Shule ya Msingi Ilala kabla ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 1981 na kujiunga na klabu ya ngumi iliyokuwa ikinolewa na kocha, Habibu Kinyogoli,” anasema Koba.
Anasema wakati huo walijifua katika gym ya Shaurimoyo, kabla ya kujiunga na klabu ya ngumi ya Simba iliyokuwa chini ya kocha Habibu Kinyogoli.
Kocha ataka asiachwe
Mwaka 1983, Koba alichaguliwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya ngumi kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya 1984.
“Nilipata nafasi hiyo baada ya kumhenyesha bingwa wa dunia wa majeshi, Nassoro Michael, pambano ambalo sitalisahau.
“Nilicheza na Nassoro aliyekuwa na rekodi ya kushinda kwa Knock Out, lakini nilimsumbua hadi raundi ya mwisho.
“Baada ya Nasoro kutangazwa mshindi, kocha mkuu wa timu ya Taifa, raia wa Bulgaria alinitangaza kuniongeza kwenye kikosi cha timu ya Taifa kwa ajili ya Olimpiki.
“Dakika tisa ambazo tulicheza na Nassoro katika pambano lile la raundi tatu ndizo ziliniweka katika ramani ya masumbwi. Nikiwa timu ya Taifa nilionekana na kuchukuliwa na Jeshi la Polisi ambalo limenipa ajira hadi sasa na kupitia kazi hiyo nimejenga,” anasema Koba ambaye ni baba wa watoto watano.
Historia ya Koba Kimanga
Mwaka 1990, Koba alitwaa ubingwa wa mashindano ya nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika ya (Press Kaba Tournament), pia amewahi kutwaa medali ya fedha ya mashindano hayo ya mwaka 1986 na 1988 na medali kama hiyo kwenye mashindano ya Afrika Mashariki ya 1994 jijini Nairobi, Kenya.

Post a Comment

أحدث أقدم