Vijana NCCR-Mageuzi wamtaka mhadhiri UDSM urais.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
 Vijana wa Chama cha NCCR-Mageuzi, wamempendekeza Dk. George Kahangwa, Mhadhiri  wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, vijana hao walisema Dk. Kahangwa ni miongoni  mwa watu ambao walibainika kuwa na sifa kati ya watu waliofikiliwa na kitengo cha vijana cha Chama hicho.
Mwingine ambaye waliesema waliona anafaa ni Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia (pichani), ambaye baada ya kumuomba kuwania nafasi hiyo hakuwa tayari na kueleza kuwa kwa sasa Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro  linahitaji msaada wake.
Mwenyekiti wa Kitengo cha Vijana Taifa, Deo Meck, alisema wanaamini Dk. Kahangwa atakuwa ni miongoni wa wagombea wazuri wa nafasi hiyo,  watakao pambanishwa katika   Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Meck alisema Dk. Kahangwa amekuwa mwanachama na mwanamageuzi wa siku nyingi,  ni msomi wa kiwango cha juu na mwenye vipaji vingi  visivyofungwa na mipaka ya taaluma na ana sifa za uongozi.
“Tumeamua kuwa licha ya  kumwomba akubaliane na pendekezo letu, tumefanya kama surprise (kushtukiza) ya kumuomba agombee nafasi hii pasipo kumshirikisha kwanza kwa sababu tunaamini kwamba ni mzalendo hawezi kukataa,  tukitoka tutaenda moja kwa moja nyumbani kwake kumpelekea taarifa hizi,” alisema Meck.
Aliongeza: “Tutafanya jitihada za kuhakikisha jina lake linafika katika kikao cha Halmashauri ya chama,  kupewa baraka za mkutano mkuu wa chama, sisi vijana tutamchukulia fomu ya chama ya kuwania nafasi hiyo muda utakapofika na tutalipa  wenyewe na hatimaye aende kushindanishwa  na wagombea na wengine wa Ukawa.”
Meck alisema uamuzi wa vijana hao wa kupendekeza mgombea wanayemtaka ni wa kwao binafsi na si wa chama, na haimaanishi kuwa   wengine wasijitokeze kuwania nafasi hiyo.
“Ieleweke kwamba sisi  kama vijana tumeamua kupendekeza mtu tunayeona anatufaa kulingana na sifa alizonazo,  haimanishi kwamba tunawafungia watu wengine milango wanaohitaji kuwania,” alisema.

Post a Comment

أحدث أقدم