Dar. Maambukizi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) yameendelea
kushika kasi nchini ambapo Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya 22 duniani
kwa kuwa na wagonjwa wengi wa TB huku ikishika nafasi ya sita kwa kuwa
na wagonjwa wengi wa TB barani Afrika.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii Dk Seif Rashidi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Donan Mmbando
alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa mwaka 2013 wagonjwa
wa Kifua Kikuu 65,000 waligunduliwa.
Alizitaja aina mbili za Kifua kikuu ikiwamo cha
mapafu ambacho hushambulia mapafu pekee na cha nje ya mapafu, huku
akibainisha kuwa cha mapafu ndiyo kinaongoza hapa nchini.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za kawaida
zinazopatikana kutoka katika vituo vya kutolewa huduma za afya ,
zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yanatokea miongoni mwa rika la vijana
wenye umri kati ya miaka 25 na 44, kama ilivyo Virusi Vya Ukimwi.
“Kifua Kikuu ni tatizo na kinashambulia zaidi
vijana ambao ndiyo tegemeo la taifa hili, hivyo kudhoofisha uchumi wa
nchi, hivyo wizara ili kunusuru kizazi hicho inaongeza juhudi za
kuhakikisha inatokomeza kama siyo kukimaliza kabisa, alisema Mmbando.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya
Duniani (WHO), kati ya watu milioni tisa wanaougua ugonjwa huo duniani
kwa mwaka, theluthi moja ya hao hawatambuliki katika mifumo ya sekta ya
afya, huku sehemu ya hao milioni tatu wanaishi katika nchi masikini
ikiwamo Tanzania.
Alisema kwa Tanzania watu wanaoshambuliwa zaidi na
ugonjwa huo ni katika makundi maalumu kama vile watu wanaoishi na
Virusi vya Ukimwi, watoto, wazee, wafungwa na watu wenye magonjwa ya
muda mrefu kama saratani na kisukari.
Meneja Mipango wa Wizara hiyo Dk. Beatrice
Mutayoba alisema kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa kudhibiti ugonjwa
huo bado ni tatizo kwa jamii na kila mwaka wagonjwa wapatao 63, 000
hugundulika. Huku Mikoa kama Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Mbeya,
Morogoro, Mara, Arusha na Tanga ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi.
“Hadi sasa kuna changamoto wa kuwabaini wagonjwa
wa kifua kikuu, kwani kati ya wagonjwa 65,732 waliobainika katika
takwimu za Kitaifa za kubaini wagonjwa zilizofanyika mwaka 2012, sawa na
asilimia 54 pekee huku wagonjwa 56,000 hukosa kugundulika na kupata
matibabu hivyo kuendelea kuwaambukiza wengine, ”alisema Dk. Mutayoba.
Dk Mutayoba pia aliwataka wananchi kutodharau
kifua cha aina yoyote kwa sababu hakuna kifua cha kawaida, hivyo kila
anayekohoa anahitaji kupata ushauri wa daktari na vipimo.
“Kifua siyo ugonjwa wa kurithi, kinaambukizwa,
kina tiba na kinapona kabisa, hivyo kila anayekohoa anahitaji kupata
tiba na vipimo sahihi badala ya kuona ni cha kawaida, ”alisema Mutayoba.
Post a Comment