Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu juzi alitumia
dakika 125 kupinga muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa wakati Bunge
lilipokaa kama kamati kupitisha vipengele.
Lissu, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alikuwa na
kazi ngumu ya kupambana na Naibu Waziri wa Sheria, Mwanasheria Mkuu na
baadhi ya wabunge wa CCM waliokuwa wakijaribu kusaidia kupitishwa kwa
muswada ambao hata hivyo ulikwama kutokana na idadi ndogo ya wabunge
waliokuwa ukumbini.
amoja na uwingi huo wa wapinzani wake, Lissu
hakuonekana kukata tamaa wala kuingia hasira zaidi ya kumwambia
Mwanasheria Mkuu, George Masaju, “stoop!” kutokana na kuchukua jukumu la
kulishauri Bunge, kitendo ambacho Lissu alisema kinamkera kwa kuwa AG
ni mshauri wa Serikali na si Bunge.
Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema
na kaimu kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, alipinga vifungu vyote
44 vya muswada huo, akisema kuwa unamuondolea mamlaka Rais ya kutangaza
hali ya hatari, sheria mpya kudurufishwa bila ya kuwa na upya wowote na
kwamba inavunja Katiba ya nchi.
Mvutano huo ulianza saa 12:00 jioni, lakini
ulishika kasi kuanzia saa 1:25 hadi 3:25 usiku baada ya Bunge zima kukaa
kama kamati kwa ajili ya kupitisha kufungu kimoja kimoja cha muswada
huo, huku Lissu akisimama mara 19 kupinga kupitishwa kwa vifungu hivyo,
akieleza kasoro zake na kushauri jinsi vinavyotakiwa kuwekwa, huku
vingine akitaka vifutwe kabisa.
Kutokana na kuibuka kwa ubishani mkali na mrefu
kati ya mbunge huyo, Masaju, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera
na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia
na kusababisha muda kuyoyoma jambo lililomfanya mwenyekiti wa Bunge,
Musa Azzan Zungu kulazimika kulihoji Bunge ili kupitisha vifungu husika.
Hata baadhi ya wabunge waliosimama kupinga hoja za
Lissu, akiwamo mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, Henry
Shekifu (Lushoto, CCM) na kutoa ufafanuzi wa kisheria, hawakuweza
kuzipangua hoja za mbunge huyo wa Singida Mashariki.
Wakati Lissu akianza kutoa ufafanuzi wa vifungu
hivyo, mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali naye alikuwa
ama akiunga mkono hoja za Lissu au kuja na hoja zake za kupinga muswada
huo.
Hata hivyo, mbunge huyo baadaye alikata tamaa na
kusema kuwa hana sababu ya kupoteza nguvu zake kutoa maoni ya msingi,
mwisho wa siku yanapuuzwa na Serikali ambayo ilikataa kila pendekezo la
wabunge hao.
“Nashangaa Mkosamali unakata tamaa,” alisema Lissu
baada ya mbunge huyo kusema hawezi kuendelea kutoa hoja zaidi za
kupinga muswada huo.
Wakati Mhagama akieleza kuwa sheria hiyo itasaidia
wanaokumbwa na maafa na kukosa msaada, kutofautisha maafa na hatari
ambazo kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Kudhibiti Maafa ya Mwaka 1990,
zinatakiwa kushughulikiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Lissu alisema
muswada huo hauna jipya.
Ilivyokuwa(Mwananchi)
إرسال تعليق