Vijana wa Chama cha NCCR-Mageuzi, wamempendekeza
Dk. George Kahangwa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
vijana hao walisema Dk. Kahangwa ni miongoni mwa watu ambao walibainika
kuwa na sifa kati ya watu waliofikiliwa na kitengo cha vijana cha Chama
hicho.
Mwingine ambaye waliesema waliona anafaa ni Mwenyekiti wa chama
hicho, James Mbatia (pichani), ambaye baada ya kumuomba kuwania nafasi
hiyo hakuwa tayari na kueleza kuwa kwa sasa Jimbo la Vunjo, mkoani
Kilimanjaro linahitaji msaada wake.
Mwenyekiti wa Kitengo cha Vijana Taifa, Deo Meck, alisema wanaamini
Dk. Kahangwa atakuwa ni miongoni wa wagombea wazuri wa nafasi hiyo,
watakao pambanishwa katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Meck alisema Dk. Kahangwa amekuwa mwanachama na mwanamageuzi wa
siku nyingi, ni msomi wa kiwango cha juu na mwenye vipaji vingi
visivyofungwa na mipaka ya taaluma na ana sifa za uongozi.
“Tumeamua kuwa licha ya kumwomba akubaliane na pendekezo letu,
tumefanya kama surprise (kushtukiza) ya kumuomba agombee nafasi hii
pasipo kumshirikisha kwanza kwa sababu tunaamini kwamba ni mzalendo
hawezi kukataa, tukitoka tutaenda moja kwa moja nyumbani kwake
kumpelekea taarifa hizi,” alisema Meck.
Aliongeza: “Tutafanya jitihada za kuhakikisha jina lake linafika
katika kikao cha Halmashauri ya chama, kupewa baraka za mkutano mkuu wa
chama, sisi vijana tutamchukulia fomu ya chama ya kuwania nafasi hiyo
muda utakapofika na tutalipa wenyewe na hatimaye aende kushindanishwa
na wagombea na wengine wa Ukawa.”
Meck alisema uamuzi wa vijana hao wa kupendekeza mgombea
wanayemtaka ni wa kwao binafsi na si wa chama, na haimaanishi kuwa
wengine wasijitokeze kuwania nafasi hiyo.
“Ieleweke kwamba sisi kama vijana tumeamua kupendekeza mtu
tunayeona anatufaa kulingana na sifa alizonazo, haimanishi kwamba
tunawafungia watu wengine milango wanaohitaji kuwania,” alisema.
Post a Comment