Wakati serikali ikiendelea kusisitiza kuwa kura ya
 maoni ya kukubali au kukataa katiba inayopendekezwa itafanyika mwezi 
ujao, vyama vya siasa vimelalamika kutopewa nakala ya katiba hiyo hadi 
sasa.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray, alisema
 vyama hivyo havijapewa nakala ya katiba inayopendekezwa licha ya 
serikali kuahidi kuitoa kwa wakati kwa wadau vikiwamo vyama hivyo.
“Nimekuwa nikipigiwa na baadhi ya vyama vya siasa vikilalamika 
kwamba  havijapewa katiba inayopendekezwa, nashangaa mamlaka 
zinazohusika hadi sasa kushindwa kutoa nakala hizo wakati muda wa kupiga
 kura ya maoni umekaribia,” alisema.
Mziray alisema serikali inapaswa kutambua kuwa vyama vya siasa ni 
wadau muhimu katika suala la katiba hivyo vilistahili kupewa nakala ya 
katiba hiyo ili vianze mchakato wa kuelimisha wananchi.
Alisema Baraza la Vyama vya Siasa linatarajia kukutana hivi 
karibuni kwa ajili ya mambo kadhaa nchini kama uandikishaji wapiga kura 
kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa alama za vidole (BVR) 
ambao umezua malalamiko mengi kutoka kwa wadau.
Lingine litakalojadiliwa ni kura ya maoni ya kukubali  au kukataa 
katiba inayopendekezwa ili vyama viweke msimamo mmoja ambao utaiweka 
nchi katika hali ya amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 
mwaka huu.
Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Omega Ngole, akithibitisha 
kuwa vyama vya siasa havijapewa nakala ya katiba na kwamba kwa sasa 
mchakato wa kuvigawia umeanza.
Ngole alisema awamu ya kwanza katiba hiyo zilisambazwa kwa mikoa, 
wilayani hadi ngazi ya mitaa na hatua itakayofuata ni kwa vyama vya 
siasa, taasisi na makundi mbalimbali.
“Unavyoongea na mimi hivi sasa tunajadiliana namna ya kuweka 
utaratibu wa kugawa katiba kwa taasisi, vyama vya siasa na makundi 
mengine, kazi hiyo inatarajia kuanza hivi karibuni,” alisema.

Post a Comment