Mwenyekiti  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serilali (PAC) 
na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, amejibu tuhuma 
zilizoelekezwa kwake na Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, 
kwamba naye amekuwa akipokea misaada mbalimbali kwa matumizi binafsi 
kuwa ni upuuzi.
Zitto alijibu tuhuma hizo jana kupitia ukurasa wake wa Facebook, 
ikiwa ni siku moja baada ya Ngeleja kumtuhumu na kueleza kuwa tuhuma 
hizo ni za kipuuzi na kwamba ameshawahi kuzijibu huko nyuma na kuziita 
ni siasa za majitaka.
“Tuhuma zote hizo zimeshawahi kutolewa huko nyuma, hazina msingi 
wowote na zilikuwa siasa za majitaka, hata hivyo zimekuwa zikijirudia 
rudia kwa malengo maalumu wanayoyajua wanaotoa tuhuma hizo” alisema 
Zotto na kuongeza:
 “Watuhumiwa wa ufisadi wa Escrow hawajazoea kuona taasisi za 
maadili zikifanya kazi kwa namna ilivyo sasa, hivyo wanajaribu na 
wataendelea kubwabwaja na kuhangaika ikiwamo kutaka kila mtu aonekane ni
 mtuhumiwa kama wao.”
“Ndiyo maana Ngeleja ametaja msururu wa watu akiwamo mfanyabiashara
 kwamba huwapa fedha wabunge bila kuwapo chembe ya ushahidi, hivyo 
narudia kutamka kwamba ninataka uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ufanyike 
mara moja, wenye ushahidi wapeleke katika vyombo vya uchunguzi na niitwe
 mbele ya Baraza la Maadili kujieleza,” alisema Zitto.
Aidha, Zitto aliunga mkono kazi iliyofanywa na Baraza la Maadili, 
alieleza kazi hiyo ilipaswa kuwa imefanywa kwa muda mrefu sasa kwa 
kashfa mbalimbali zilizowahi kuwapata viongozi, kama vile rada, rushwa 
katika manunuzi ya mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya umeme, 
kujipatia mikopo katika taasisi za umma bila kulipa na kujilimbilikizia 
mali tofauti na kipato.
Zitto aliiomba Sekretarieti ya Maadili izichukulie kwa uzito tuhuma
 za Ngeleje dhidi yake, kwani kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi
 wa umma yanapaswa yafanyiwe uchunguzi. 
Akijitetea juzi kwenye Baraza la Maadili, Ngeleja alikiri kupata 
mgawo wa Sh. bilioni 40.2 kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemalila wa 
kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd na kudai kuwa wabunge 
wamekuwa wakifadhiliwa na wafanyabiashara na  mmoja wa wabunge 
walionufaika na misaada ya fedha za wafadhili, ni Zitto, ambaye kisheria
 ni mtumishi wa umma.
Alidai Zitto alinufaika na msaada wa zaidi ya Sh. milioni 30 na 
dola za Marekani 5,000 kutoka kwa Kampuni ya Pan Africa Power (PAP) na 
Independent Power Tanzania Limited (IPTL) alizopata kwa matumizi yake 
binafsi.
Ngeleja alidai misaada mingine, ambayo Zitto amewahi kuipata ni 
pamoja na unaohusu Sh. milioni 119.9 na Sh. milioni 79, ambayo alidai 
kuwa aliipata kutoka Shirika la Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)

Post a Comment