Wasafiri kadhaa raia wa Cameroon wameripotiwa kutekwa nyara na watu
wasiojulikana karibu na mpaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Duru za
kuaminika zimeripoti kuwa, watu hao 15 wametekwa nyara na watu wenye
silaha wa kundi linaloongozwa na mtu mmoja anayetambulika kwa jina la
Abdoulaye Miskine, huko kaskazini mashariki mwa Cameroon karibu na mpaka
wa pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Chanzo kimoja cha usalama nchini Cameroon kimeeleza kuwa, wasafiri
hao 15 walitekwa nyara usiku wa Alkhamis iliyopita katika kijiji cha
Gbabio kilichoko umbali wa kilometa 10 kutoka mji wa Garoua-Boulaï,
mashariki mwa Cameroon.
Chanzo hicho ambacho hakikutaka kutaja jina lake kimesema kuwa, bila
shaka yoyote raia hao wa Cameroon walitekwa nyara na wanachama wa kundi
la Abdoulaye Miskine ambalo ni maarufu kwa vitendo vya ukatili na
machafuko mashariki mwa taifa hilo.
Kwa mujibu wa jeshi la polisi la Cameroon, wasafiri hao walitekwa
nyara majira ya saa 11 za usiku kutoka katika mji wa Bertoua, makao
makuu ya mkoa wa mashariki mwa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa mwaka
uliopita, Abdoulaye Miskine alitiwa mbaroni karibu na mpaka wa Cameroon
na Jamhuri ya Afrika ya Kati na kufungwa jela miezi kadhaa.
CHANZO: BBC SWAHILI
إرسال تعليق