Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira aliyepewa
jukumu la kuandaa Ilani ya CCM kwa ushirikiano na timu ya watu 23 wa
chama hicho itakayotumia kwenye kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 hadi
2020, amejitokeza na kusema kazi hiyo ipo ukingoni kukamilika.
Kauli hiyo Wasira ameitoka siku moja baada ya
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuwaeleza waandishi wa
habari mjini Arusha kuwa Ilani hiyo inasimamiwa na Wasira na inatarajia
kutoa Dira ya Mwelekeo ya chama hicho tawala katika kutatua matatizo ya
wananchi.
Alisema Ilani hiyo itaangazia pia mambo ambayo
yaliahidiwa ndani ya Ilani iliyopita na hayakutekelezwa ipasavyo. Baadhi
ya mambo ambayo hayakufanikiwa ni tatizo la maji, migogoro ya ardhi na
suala la ajira.
Akizungumza jana na gazeti hili kwa njia ya simu,
Wasira alisema: “Unajua labda ninyi mtakuwa mmechelewa kupata taarifa
kuwa tumeanza lini, lakini sisi tulikwishaanza kazi hii na tuko hatua za
mwisho za kutoa Rasimu ya Ilani yenyewe.”
Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda alisema Ilani
hiyo inaandaliwa kwa kuangalia changamoto gani zilizojitokeza kwa miaka
10 nyuma na ndiyo wanayoipa kipaumbele katika maandalizi hayo.
“Ukiangalia uchumi umekuwa ukikua kwa asilimia
saba kila mwaka lakini si kiwango kikubwa ukilinganisha na maisha ya
wananchi yalivyo hivyo Ilani hii itatakiwa kuja na majibu ya tatizo hilo
na kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na maisha bora,” alisema Wasira.
“Suala la ajira ukiangalia wanafunzi wengi
wanaanza shule za msingi na wanapomaliza wanaendelea sekondari na baada
ya hapo wanakwenda vyuoni hivyo wahitimu wa vyuo vyetu wanaongezeka
jambo hapa ni kuja na mkakati wa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana
wetu.”
Post a Comment