Wasira: Ilani ya CCM iko mbioni kukamilika

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira aliyepewa jukumu la kuandaa Ilani ya CCM kwa ushirikiano na timu ya watu 23 wa chama hicho itakayotumia kwenye kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 hadi 2020, amejitokeza na kusema kazi hiyo ipo ukingoni kukamilika.
Kauli hiyo Wasira ameitoka siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuwaeleza waandishi wa habari mjini Arusha kuwa Ilani hiyo inasimamiwa na Wasira na inatarajia kutoa Dira ya Mwelekeo ya chama hicho tawala katika kutatua matatizo ya wananchi.
Alisema Ilani hiyo itaangazia pia mambo ambayo yaliahidiwa ndani ya Ilani iliyopita na hayakutekelezwa ipasavyo. Baadhi ya mambo ambayo hayakufanikiwa ni tatizo la maji, migogoro ya ardhi na suala la ajira.
Akizungumza jana na gazeti hili kwa njia ya simu, Wasira alisema: “Unajua labda ninyi mtakuwa mmechelewa kupata taarifa kuwa tumeanza lini, lakini sisi tulikwishaanza kazi hii na tuko hatua za mwisho za kutoa Rasimu ya Ilani yenyewe.”
Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda alisema Ilani hiyo inaandaliwa kwa kuangalia changamoto gani zilizojitokeza kwa miaka 10 nyuma na ndiyo wanayoipa kipaumbele katika maandalizi hayo.
“Ukiangalia uchumi umekuwa ukikua kwa asilimia saba kila mwaka lakini si kiwango kikubwa ukilinganisha na maisha ya wananchi yalivyo hivyo Ilani hii itatakiwa kuja na majibu ya tatizo hilo na kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na maisha bora,” alisema Wasira.
“Suala la ajira ukiangalia wanafunzi wengi wanaanza shule za msingi na wanapomaliza wanaendelea sekondari na baada ya hapo wanakwenda vyuoni hivyo wahitimu wa vyuo vyetu wanaongezeka jambo hapa ni kuja na mkakati wa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu.”

Post a Comment

أحدث أقدم