Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema wamekosoa taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupata hati zenye
mashaka na kueleza kuwa hesabu za vyama vyao zipo sahihi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye na Mkurugenzi wa Fedha wa
Chadema, Anthony Komu walidai taarifa ya CAG ndiyo yenye upungufu.
Nape katika mahojiano maalumu na waandishi wa
habari yaliyorushwa moja kwa moja na kituo cha Radio 5 Arusha alisema,
kuna tatizo la kutokubaliana kutokana na ukaguzi wa CAG.
Alisema mahesabu ya CCM yanayotokana na fedha za
ruzuku kutoka serikalini yapo sahihi lakini wana mgogoro na CAG ambaye
anataka mahesabu juu ya mali zote za CCM.“CCM ina miradi mingi kwa mfano
hapa Arusha tuna uwanja wa Sheikh Amri Abeid awali uwanja huu, ulikuwa
unasimamiwa na Mkoa wa Arusha pekee, sasa mkoa umegawanywa siyo rahisi
kuwa na mahesabu yote,” alisema.
Alisema kwa maagizo ya CAG, kuandaa hesabu na
taarifa za mali zote za CCM, inahitaji kutumika kwa zaidi ya Sh1 bilioni
jambo ambalo ni gumu.
“Sisi tunadhani CAG anapaswa kukagua mahesabu ya
fedha za ruzuku tunazopewa na Serikali lakini siyo mahesabu ya mali zote
za CCM,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, ameainisha vigezo
saba tofauti vilivyosababisha hesabu za CCM kupata hati yenye mashaka na
kueleza kuwa CCM imekosa uhalali wa kisheria kumiliki baadhi ya mali
ilizonazo.
Ukaguzi huo wa CAG umefanyika kwa mujibu wa Sheria
namba 5 ya mwaka 1992 ya Vyama vya Siasa, iliyofanyiwa marekebisho na
Sheria namba 7 ya mwaka 2009, inayompa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za
vyama vya siasa.
Ilibainisha vigezo vingine vya hati yenye mashaka
kuwa ni CCM kutowasilisha taarifa ya mapato yake ya fedha kutoka kwa
wafadhili mbalimbali zilizofikia Sh1,526,536,802, huku CAG pia
akishindwa kupata nyaraka za kuthibitisha matumizi na malipo
yaliyofanywa na chama hicho yanayofikia Sh6,045,438,052.
Kwa upande wa Chadema, Komu alisema ripoti ya CAG
ina upungufu kwani, inataka chama hicho kuandaa taarifa za mahesabu na
uthamini wa mali hadi mikoani.
“Mapungufu (upungufu) ambayo alianisha ya
kutofanya uthamini wa mali zetu kutokuwa na mahesabu ya benki katika
ngazi mbalimbali na vitabu vya risiti kwa baadhi ya maeneo ni mambo
ambayo huwezi kuyakamilisha kutokana na mfumo wa vyama vyetu,” alisema.
Alikiri kuwa chama kuwa na akaunti nyingi kwa madai kuwa kila mkoa, wilaya na jimbo wana akauti yao.(Mwananchi)
إرسال تعليق