Hii ni mara ya pili katika muda usiozidi wiki moja
baada ya polisi kubaini nyumba iliyohifadhi watoto 18 kwa lengo kama
hilo Jumamosi iliyopita.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela
alisema tukio hilo linafanya wapelelezi kuumiza vichwa kwa kuwa mikoa
waliyotoka ndio ile ile waliyotoka watoto 18 waliokutwa kwenye nyumba
moja mjini Moshi.
Nyumba hiyo imebainika wakati kukiwa na madai
kwamba baadhi ya misikiti katika maeneo ya Pasua, Njoro na Kibosho
yanaendesha mafunzo ya judo na karate.
Kamanda Kamwela alieleza kuwa kama ilivyokuwa
awali, watoto waliobainika juzi wanatoka katika mikoa ya Tanga, Dodoma,
Singida, Tabora na Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, watoto hao waligunduka
katika nyumba iliyoko eneo la Lyamungo wilayani Hai. Alisema umri wao
ni kati ya miaka 14 na 17 na walikuwa wanafundishwa dini na ushonaji.
Alisema kituo hicho ambacho hakijasajiliwa,
kinaitwa Umm Sukhail na kinamilikiwa na mwalimu mstaafu, Abubakar Juma
(64) mkazi wa Tanga ambaye kwa sasa anaishi maeneo ya Kibosho Mweka.
Kamwela alisema watoto hao wamechukuliwa na polisi
kwa uchunguzi zaidi ili kujua sababu za wao kuishi katika eneo hilo pia
kubaini ukweli wa mafunzo yanayotolewa kwenye kituo hicho.
“Kutokana na kugundulika kwa mafunzo haya yasiyo
rasmi yanayotolewa na walimu ambao pia si rasmi, lazima tuchunguze kama
baada ya kuhitimu wanapewa vyeti na wanafanya kazi wapi,” alisema.
Kamwela pia alisema polisi wanafanya uchunguzi ili
kubaini kama watoto hao walipata elimu ya msingi kama sheria
inavyoelekeza na kama walifaulu ama la na kwanini hawakuendelea na
masomo. Kamanda alisema upo uwezekano wa watoto 18 waliokutwa Pasua
kuhamishiwa kituo cha Narumu na kwamba jeshi hilo linaendelea na
uchunguzi kubaini kama wenye vituo hivyo wanafanya kazi pamoja.
Kuhusu watoto 18 wa Pasua, Kamanda Kamwela alisema
wametambuliwa na wazazi wao na kuchukuliwa, lakini bado uchunguzi
unaendelea kujua uhusiano wao na mmiliki wa nyumba hiyo.
“Tunachunguza kujua kama wazazi walikuwa
wakifahamu maisha wanayoishi na sababu za kuwatoa kwenye shule za
Serikali na kuwapeleka kwenye shule za dini wakati elimu ya msingi ni ya
lazima,” alisema
- Mwananchi

Post a Comment