Watoto wengine 11 wakutwa wamefichwa

Moshi. Mambo mazito zaidi yamezidi kubainika mkoani Kilimanjaro baada ya polisi kugundua nyumba nyingine yenye watoto kumi na mmoja waliokusanywa kutoka mikoa mbalimbali kwa ajili ya kufundishwa dini.
Hii ni mara ya pili katika muda usiozidi wiki moja baada ya polisi kubaini nyumba iliyohifadhi watoto 18 kwa lengo kama hilo Jumamosi iliyopita.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela alisema tukio hilo linafanya wapelelezi kuumiza vichwa kwa kuwa mikoa waliyotoka ndio ile ile waliyotoka watoto 18 waliokutwa kwenye nyumba moja mjini Moshi.
Nyumba hiyo imebainika wakati kukiwa na madai kwamba baadhi ya misikiti katika maeneo ya Pasua, Njoro na Kibosho yanaendesha mafunzo ya judo na karate.
Kamanda Kamwela alieleza kuwa kama ilivyokuwa awali, watoto waliobainika juzi wanatoka katika mikoa ya Tanga, Dodoma, Singida, Tabora na Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, watoto hao waligunduka katika nyumba iliyoko eneo la Lyamungo wilayani Hai. Alisema umri wao ni kati ya miaka 14 na 17 na walikuwa wanafundishwa dini na ushonaji.
Alisema kituo hicho ambacho hakijasajiliwa, kinaitwa Umm Sukhail na kinamilikiwa na mwalimu mstaafu, Abubakar Juma (64) mkazi wa Tanga ambaye kwa sasa anaishi maeneo ya Kibosho Mweka.
Kamwela alisema watoto hao wamechukuliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi ili kujua sababu za wao kuishi katika eneo hilo pia kubaini ukweli wa mafunzo yanayotolewa kwenye kituo hicho.
“Kutokana na kugundulika kwa mafunzo haya yasiyo rasmi yanayotolewa na walimu ambao pia si rasmi, lazima tuchunguze kama baada ya kuhitimu wanapewa vyeti na wanafanya kazi wapi,” alisema.
Kamwela pia alisema polisi wanafanya uchunguzi ili kubaini kama watoto hao walipata elimu ya msingi kama sheria inavyoelekeza na kama walifaulu ama la na kwanini hawakuendelea na masomo. Kamanda alisema upo uwezekano wa watoto 18 waliokutwa Pasua kuhamishiwa kituo cha Narumu na kwamba jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kubaini kama wenye vituo hivyo wanafanya kazi pamoja.
Kuhusu watoto 18 wa Pasua, Kamanda Kamwela alisema wametambuliwa na wazazi wao na kuchukuliwa, lakini bado uchunguzi unaendelea kujua uhusiano wao na mmiliki wa nyumba hiyo.
“Tunachunguza kujua kama wazazi walikuwa wakifahamu maisha wanayoishi na sababu za kuwatoa kwenye shule za Serikali na kuwapeleka kwenye shule za dini wakati elimu ya msingi ni ya lazima,” alisema
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم