Askari wa Chad na Niger wakiwa Damasak.
Makumi ya miili ya watu wanaosadikiwa kuuawa na wanachama wa kundi la
kigaidi na kitakfiri wa Boko Haram, imegunduliwa katika Mji wa Damasak
uliopo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Taarifa zinaeleza kuwa, miili hiyo ya watu 70 ambayo mingi kati yake
imekutwa ikiwa imekatwa vichwa, imegunduliwa na askari wa Chad na Niger
katika mji huo wa Damasak nchini humo. Tayari uchunguzi umeanzishwa kwa
lengo la kuwatambua wahusika wa ukatili huo, ingawa kidole cha lawama
tayari kimeelekezwa kwa wanachama wa kundi la kitakfiri la Boko Haram,
ambalo limekuwa likitekeleza mauaji kama hayo.
Hadi siku ya Jumamosi iliyopita, ambapo askari hao wa Chad na Niger
waliuvamia mji huo na kuukomboa kutoka kwa wanachama wa kundi la Boko
Haram, ulikuwa umetelekezwa kabisa na serikali ya Nigeria.
Tangu mwezi Novemba mwaka jana ambapo mji huo ulidhibitiwa na kundi
hilo, wakazi wake walikuwa wakijaribu kutoroka ingawa hata hivyo
walikuwa wakizuiliwa na magaidi hao wanaotekeleza jinai kwa jina la
Uislamu.
Inaelezwa kwamba, baada ya mji huo kudhibitiwa na kundi hilo,
wanachama wake walivamia maduka na makazi ya watu na kupora kila
walichokitaka, huku wakiwabaka na kuwanajisi wanawake na wasichana wa
mji huo.
CHANZO: BBC NEWZ
إرسال تعليق