YANGA inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kesho Jumatano
inaanza mwezi mgumu wa April ambapo ikicheza karata zake vizuri
itajihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani,
lakini ni mwezi wa kutengeneza heshima pia kwa Mwarabu.
Ni mwezi ambao Yanga kama ikiimaliza FC Platinum
ya Zimbabwe ina uwezekano mkubwa wa kukutana na Etoile du Sahel ya
Tunisia, ambayo ni moja ya timu ngumu za kiarabu zinazosumbua Waswahili
lakini mwezi huo ndiyo ambao Yanga inaweza kujijengea au kujiharibia.
Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 40 huku
ikihitaji kushinda mechi nne tu kujihakikishia kushiriki tena michuano
hiyo tofauti na Simba ambayo hata ikishinda mechi zote sita zilizobaki
itafikisha pointi 50 wakati Yanga waliobakiza mechi saba watafikisha
pointi 53 kwa kushinda mechi nne.
Mwezi ujao, Yanga itakuwa na mechi tatu kama
hakutakuwa na mabadiliko yoyote kwenye ratiba ya ligi wakati Simba wao
watacheza mechi nne ambapo mbili zitachezwa nyumbani na nyingine mbili
ugenini kati ya Kagera Sugar itakayochezwa Uwanja wa Kambarage mkoani
Shinyanga Jumamosi na ile ya Aprili 18 dhidi ya Mbeya City itakayochezwa
Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mechi za nyumbani ni dhidi ya Mgambo Shooting
itakayochezwa wiki ijayo, April 12 na ile ya Ndanda United itakayochezwa
April 25, zote zitapigwa Uwanja wa Taifa. Mechi zote ni ngumu kwa Simba
kwani wanapaswa kucheza kila wiki.
Yanga wenyewe mwezi ujao mechi zote zitachezwa
nyumbani Uwanja wa Taifa ambapo wakirejea kutoka Zimbabwe wataanza na
Mbeya City, Coastal Union na Ruvu Shooting.
Kwa kufuata hesabu za msimamo wa ligi, Yanga bado
wataendelea kutesa mwezi ujao kama watashinda mechi zote tatu na
kukusanya pointi 49 na kama watapoteza mechi bado wataizidi Simba ambao
hata wakishinda mechi zote nne watafikisha pointi 44 hata kama Yanga
watapoteza moja Simba hawatafikia pointi za Yanga kwa mwezi huu.
Yanga wanatarajia kuondoka usiku wa kuamkia
keshokutwa Alhamisi kwenda kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Platinum
ya Zimbabwe ambapo mechi ya awali Yanga ilishinda mabao 5-1 wakati Simba
wao wataondoka kesho Jumatano kuelekea Shinyanga kuwafuata Kagera
Sugar.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa ni mwezi mmoja na
ushei Simba imetoka kupokea kichapo cha bao 1-0 mjini Shinyanga mbele ya
Stand United katika uwanja utakaowakutanisha na Kagera Sugar yaani CCM
Kambarage.
Post a Comment