Askofu Benson Bagonza
Joseph Ngilisho, Arusha
LILE sakata la Peace Sylvester (36), mkazi wa Kijenge jijini
hapa kudai amezaa watoto wawili na Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera
limechukua sura mpya baada ya Peace kuibua mambo mapya.
Akizungumza na gazeti hili Jumamosi iliyopita, Peace alisema kuwa,
amefuatwa na mtu aliyedai ametumwa na askofu huyo kumpa shilingi 400,000
kama nauli ya kwenda kwao Karagwe kwa ajili ya suluhu na askofu huyo.
Pia Peace alibainisha kwamba, baadhi ya viongozi wa kanisa hilo
wanafanya mipango ya chini kwa chini kwa kuwatumia baadhi ya waandishi
wa habari ili kukutana naye kwa lengo la kumshawishi akanushe taarifa
iliyotoka kwenye gazeti hili Jumatatu iliyopita.
“Kuna mwandishi wa habari anaitwa…(anamtaja jina) amekuja hapa Arusha
akitokea Dar kwa ajili yangu. Huyu mwandishi amekuwa akinipigia simu
mara kwa mara akitaka tukutane ili anishawishi nikanushe zile habari
nilizotoa kwamba nimezaa na askofu na amenitelekezea watoto, anasema
ametumwa na uongozi,” alisema Peace.
Aliendelea kusema kuwa, baada ya habari hiyo kutoka baadhi ya ndugu
zake waliopo Karagwe waliandika barua kwenda Kituo Kikuu cha Polisi
Arusha wakisema kwamba, ukoo umekaa kikao na kuamua kutomtambua Peace
kama ndugu yao.
Hata hivyo, Peace alisema mpaka sasa ndugu wamegawanyika juu ya hatua
ya kutaka kumtenga huku baadhi yao wakifunga safari kwenda jijini
Arusha kumsaidia matatizo yake na askofu.
Philemon Sylvester na Charles Sylvester ambao ni kaka wa Peace
(pichani juu) ndiyo wapo Arusha na kuliambia gazeti hili kwamba, barua
ya kumtenga Peace wao hawaitambui na kuongeza kuwa, iliandikwa na ndugu
yao mmoja kwa masilahi yake.
Peace alisema Ijumaa iliyopita aliitwa na katibu mkuu wa kanisa hilo
na kumshawishi ili akanushe taarifa hiyo hatua ambayo alisema kuwa
alimkatalia kwa vile anachotaka ni haki ya watoto wake.
Katika gazeti hili toleo la Jumatatu iliyopita, ukurasa wake wa mbele
kuliandikwa habari yenye kichwa: AIBU; ASKOFU KKKT APIGA MIMBA MBILI
NJE YA NDOA.
Katika habari hiyo, Peace ndiye mlalamikaji mkuu akidai amezalishwa
na askofu huyo watoto wawili, Piana (6) na Bariki (3) huku akitelekezewa
bila huduma.
Alisema suala hilo amelifikisha kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Arusha
na kufunguliwa jalada namba AR/RB/5290/2015 KUTELEKEZA FAMILIA.
Katika habari hiyo, askofu huyo alijitetea kwa kusema na mwandishi
wetu kwamba hajawatelekeza watoto hao ni siku za karibuni alimtumia
Peace shilingi 250,000 madai ambayo Peace alikiri kupokea kiasi hicho
cha pesa na kusema askofu alifanya hivyo baada ya yeye kufikisha
malalamiko yake kwenye dola.
Post a Comment