ALIYEDAI KUZAA NA ASKOFU MAPYA YAIBUKA

Askofu Benson Bagonza
Joseph Ngilisho, Arusha
LILE sakata la Peace Sylvester (36), mkazi wa Kijenge jijini hapa kudai amezaa watoto wawili na Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera limechukua sura mpya baada ya Peace kuibua mambo mapya.
Akizungumza na gazeti hili Jumamosi iliyopita, Peace alisema kuwa, amefuatwa na mtu aliyedai ametumwa na askofu huyo kumpa shilingi 400,000 kama nauli ya kwenda kwao Karagwe kwa ajili ya suluhu na askofu huyo.
Pia Peace alibainisha kwamba, baadhi ya viongozi wa kanisa hilo wanafanya mipango ya chini kwa chini kwa kuwatumia baadhi ya waandishi wa habari ili kukutana naye kwa lengo la kumshawishi akanushe taarifa iliyotoka kwenye gazeti hili Jumatatu iliyopita.
“Kuna mwandishi wa habari anaitwa…(anamtaja jina) amekuja hapa Arusha akitokea Dar kwa ajili yangu. Huyu mwandishi amekuwa akinipigia simu mara kwa mara akitaka tukutane ili anishawishi nikanushe zile habari nilizotoa kwamba nimezaa na askofu na amenitelekezea watoto, anasema ametumwa na uongozi,” alisema Peace.
Aliendelea kusema kuwa, baada ya habari hiyo kutoka baadhi ya ndugu zake waliopo Karagwe waliandika barua kwenda Kituo Kikuu cha Polisi Arusha wakisema kwamba,  ukoo umekaa kikao na kuamua kutomtambua Peace kama ndugu yao.
Hata hivyo, Peace alisema mpaka sasa ndugu wamegawanyika juu ya hatua ya kutaka kumtenga huku baadhi yao wakifunga safari kwenda jijini Arusha kumsaidia matatizo yake na askofu.
Philemon Sylvester na Charles Sylvester ambao ni kaka wa Peace (pichani juu)  ndiyo wapo Arusha na kuliambia gazeti hili kwamba, barua ya kumtenga Peace wao hawaitambui na kuongeza kuwa, iliandikwa na ndugu yao mmoja kwa masilahi yake.
Peace alisema Ijumaa iliyopita aliitwa na katibu mkuu wa kanisa hilo na kumshawishi ili akanushe taarifa hiyo hatua ambayo alisema kuwa alimkatalia kwa vile anachotaka ni haki ya watoto wake.
Katika gazeti hili toleo la Jumatatu iliyopita, ukurasa wake wa mbele kuliandikwa habari yenye kichwa: AIBU; ASKOFU KKKT APIGA MIMBA MBILI NJE YA NDOA.
Katika habari hiyo, Peace ndiye mlalamikaji mkuu akidai amezalishwa na askofu huyo watoto wawili, Piana (6) na Bariki (3) huku akitelekezewa bila huduma.
Alisema suala hilo amelifikisha kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Arusha na kufunguliwa jalada namba AR/RB/5290/2015 KUTELEKEZA FAMILIA.
Katika habari hiyo, askofu huyo alijitetea kwa kusema na mwandishi wetu kwamba hajawatelekeza watoto hao ni siku za karibuni alimtumia Peace shilingi 250,000 madai ambayo Peace alikiri kupokea kiasi hicho cha pesa na kusema askofu alifanya hivyo baada ya yeye kufikisha malalamiko yake kwenye dola.

Post a Comment

أحدث أقدم