JOSEPH Matitu anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 50 ambaye
hajajulikana kuwa ni mkazi wa wapi, ameokotwa na wasamaria wema Machi
13, mwaka huu baada ya kudondoka ghafla na kupoteza fahamu.
Joseph Matitu anayedaiwa kupoteza fahamu kwa miezi miwili, akiendelea kupata matibabu.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, Matitu aliokotwa Kibaha, mkoani Pwani
baada ya watu kumuona akiwa amelala chini, wakahisi alikuwa amefariki
dunia.
Hata hivyo, baada ya kumsogelea walimuona akipumua lakini akiwa
hajitambui, wakachukua jukumu la kumkimbiza katika Hospitali ya Tumbi,
Kibaha kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
AHAMISHIWA MUHIMBILI
“Mzee huyo alipofikishwa katika hospitali hiyo, madaktari walimlaza
kwa siku mbili, hata hivyo baada ya kuona hali yake inazidi kudorora,
uongozi uliamua kumhamishia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu
zaidi akiwa hajitambui,” alisema mtoa habari kwa sharti la kutoandikwa
jina gazetini.
Ilielezwa kuwa mzee huyo alianza matibabu katika hospitali hiyo Machi
16, mwaka huu lakini hadi leo hajapata ndugu zake wala anapoishi
hapajulikani.
Baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo, madaktari walianza
matibabu, hata hivyo, hali yake hadi sasa bado ni mbaya japokuwa amepata
fahamu na anaongea kwa tabu baada ya kupoteza fahamu kwa miezi miwili.
Mmoja wa wauguzi katika wodi 1 ya Mwaisela ambaye hakutaka jina
lake liandikwe gazetini, alisema mgonjwa huyo hadi sasa hawezi kuongea
japokuwa ana nafauu ukilinganisha na jinsi alivyoletwa akitokea Tumbi,
Kibaha.
Afisa Ustawi Jamii wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Grace Julius
anayesimamia Wodi 1 ya Mwaisela alisema mgonjwa huyo anaendelea vizuri.
“Hadi sasa Matitu hajapata ndugu hivyo yeyote aliyepotelewa na ndugu afike kumtambua,” alisema Grace.
Afisa Habari Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha
alisema kuwa kazi ya hospitali hiyo ni kuhakikisha kila mtu anapata
matibabu kadiri inavyowezekana awe ana ndugu au hana.
WITO KWA UMMA “Anayemfahamu Joseph Matitu ajitokeze au
awajulishe ndugu zake wa karibu kama anawafahamu au wafike Muhimbili
Wodi 1 ya Mwaisela,” alisema.
Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii awasiliane na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Muhimbili kwa namba O765 409 575.
Post a Comment