Moshi. Helkopta ya Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo,
imeleta kizaazaa, baada ya Kada wa CCM, Buni Ramolle ambaye aliikodi kwa
ajili ya mikutano yake ya kutangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo
hilo, kudai kuwa ni mbovu na ilitaka kumuua.
Kada huyo akaenda mbali na kueleza kuwa kutokana
na hitilafu hiyo, ameitaka kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd,
iliyomkodishia helkopta hiyo, kumrejeshea fedha zake zote alizoilipa
kwa ajili ya kuitumia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, Ndesamburo ambaye ni mmiliki wa
helkopta hiyo kupitia kampuni yake ya Keys Aviation, alikanusha madai
hayo akisema kuwa hayana msingi.
“Anasema helikopta ni mbovu wakati ilimpeleka na
kumrudisha? Alihoji Ndesamburo na kusisitiza kuwa “tutawaomba wakaguzi
wa ndege waifanyie ukaguzi na ripoti hiyo ndio tutaitumia kumshitaki
nayo.”
Kuhusu madai ya Ramolle kuwa amerejeshewa fedha
zake alizolipa, Ndesamburo alihoji “Tunamrudishia fedha gani wakati
hakulipa? Kuwa na Proforma Invoice ndio kulipia?”
Awali taarifa zilieleza kuwa Ramolle alitoa tuhuma
hizo, baada ya viongozi wa CCM, kumbana wakimtaka aeleze kwa nini
ameamua kutumia helkopta ya Ndesamburo ambaye ni mpinzani wake kisiasa.
Jana Ramolle alitumia mkutano wake na waandishi wa
habari kukanusha kuwa helkopta aliyoitumia Aprili 18 mwaka huu ni ya
Ndesamburo. Alidai katika mkutano huo kuwa helkopta hiyo aliikodisha
kama mteja kutoka kampuni ya General Aviation Services na hajui kama ni
ya Ndesamburo.
Lakini tayari Ndesamburo mwenyewe ameshajitokeza
hadharani na kudai kuwa helkopta hiyo ni mali yake na kwamba ameingia
mkataba wa kuikodisha kwa kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd.
Huu ni mchezo mchafu
Kwa mujibu wa Ramolle, kinachofanyika sasa ni
mbinu za kumchafua ndani ya chama ili asiaminike na aenguliwe kama
alivyoenguliwa mwaka 2010.
Ramolle alisema kutokana na Ndesamburo kudai
helkopta hiyo ni yake, tayari kampuni ya General Aviation Services
wamemrudishia fedha zake alizokuwa amekodishia na ameishtaki kampuni
hiyo kwa Meneja wa TRA mkoa wa Kilimanjaro kutokana na kutompa risiti ya
malipo aliyoyafanya. Buni alisema atapambana na waandishi wanaotaka
kumchafua kwa kuwa ana mahasimu ndani na nje ya chama na kutaka
asiharibiwe kazi yake na siasa.
“Nimechoka kunyanyaswa nimepata madhara makubwa
kwa sababu ya siasa nina maadui ndani na nje ya chama nitapambana na
yeyote atakayenizushia maneno na mtu asinifuatefuate” alisema.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment