Asasi zisizo za kiserikali 53 zimemwandikia Rais
Jakaya Kikwete, barua ya kumuomba asisaini Sheria ya Takwimu ya 2015 na
Sheria ya Makosa ya Mtandaoni zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni ili
kuruhusu kufanyiwa marekebisho kwanza.
Kwa majibu wa barua hiyo iliyosainiwa na asasi 53 na mtandao wa
asasi za kiraia ambayo NIPASHE imeona nakala yake, zinataka sheria hizo
zirudishwe bungeni kuondoa vifungu vinavyokwenda kinyume na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na haki za binadamu kwa ujumla.
“Tunashauri kabla ya kutia saini sheria hizi upate muda wa
kusikiliza kilio cha jamii juu ya ubaya wa sheria hizi kwa mustakabali
wa taifa. Sheria hizi zikipitishwa katika utawala wako zitatia doa
dhamira yako nzuri ya kuongeza wigo na uhuru wa habari na ushiriki wa
wadau katika maendeleo ya kitaifa,” alisema.
Barua hiyo imeeleza sababu za kumtaka Rais kutosaini sheria hizo
kuwa ni, malengo ya Sheria ya Takwimu siyo tu kuratibu takwimu za
kitaifa, bali umetoa madaraka makubwa kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS) kama kitovu cha utoaji wa takwimu nchini.
“Maana yake ni kwamba taasisi zote za serikali, mashirika binafsi,
taasisi za elimu ya juu, vyuo vikuu na taasisi za utafiti hazitakuwa na
uhuru wa kutoa matokeo ya tafiti wanazozifanya bila ya kibali au ridhaa
ya NBS” ilisema barua hiyo.
Imesema pia sheria hiyo imeweka adhabu kali kwa vyombo vya habari,
asasi za kiraia, taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu
vitakavyotenda makosa yaliyoainishwa katika sehemu ya tatu ya sheria.
Kuhusu Sheria ya Makosa ya Mitandao, barua hiyo imesema itaminya
kwa kiasi kikubwa uhuru wa wananchi kuwasiliana na kupashana habari
endapo itasainiwa bila marekebisho.
“Ni dhahiri sheria hii imelenga kufuta kabisa uhuru wa mawasiliano
na matumizi ya mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp, Jamii
Forums, Twitter, blog… Kupitishwa kwa sheria hii bila kufanyiwa
marekebisho kutasababisha Watanzania wengi kutiwa hatiani bila sababu,
lakini pia kutaondoa kabisa uhuru wa habari nchini” iliongeza kusema
Post a Comment