Asasi 53 zamtaka Rais asisaini Sheria ya Takwimu, Mtandao.

Rais Jakaya Kikwete.
Asasi zisizo za kiserikali 53 zimemwandikia Rais Jakaya Kikwete, barua ya kumuomba asisaini Sheria ya Takwimu ya 2015 na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni ili kuruhusu kufanyiwa marekebisho kwanza.
 
Kwa majibu wa barua hiyo iliyosainiwa na asasi 53 na mtandao wa asasi za kiraia ambayo NIPASHE imeona nakala yake, zinataka sheria hizo zirudishwe bungeni kuondoa vifungu vinavyokwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na haki za binadamu kwa ujumla.
 
“Tunashauri kabla ya kutia saini sheria hizi upate muda wa kusikiliza kilio cha jamii juu ya ubaya wa sheria hizi kwa mustakabali wa taifa. Sheria hizi zikipitishwa katika utawala wako zitatia doa dhamira yako nzuri ya kuongeza wigo na uhuru wa habari na ushiriki wa wadau katika maendeleo ya kitaifa,” alisema.
 
Barua hiyo imeeleza sababu za kumtaka Rais kutosaini sheria hizo kuwa ni, malengo ya Sheria ya Takwimu siyo tu kuratibu takwimu za kitaifa, bali umetoa madaraka makubwa kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kama kitovu cha utoaji wa takwimu nchini. 
 
“Maana yake ni kwamba taasisi zote za serikali, mashirika binafsi, taasisi za elimu ya juu, vyuo vikuu na taasisi za utafiti hazitakuwa na uhuru wa kutoa matokeo ya tafiti wanazozifanya bila ya kibali au ridhaa ya NBS” ilisema barua hiyo.
 
Imesema pia sheria hiyo imeweka adhabu kali kwa vyombo vya habari, asasi za kiraia, taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu vitakavyotenda makosa yaliyoainishwa katika sehemu ya tatu ya sheria. 
 
Kuhusu Sheria ya Makosa ya Mitandao, barua hiyo imesema itaminya kwa kiasi kikubwa uhuru wa wananchi kuwasiliana na kupashana habari endapo itasainiwa bila marekebisho. 
 
“Ni dhahiri sheria hii imelenga kufuta kabisa uhuru wa mawasiliano na matumizi ya mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp, Jamii Forums, Twitter, blog… Kupitishwa kwa sheria hii bila kufanyiwa marekebisho kutasababisha Watanzania wengi kutiwa hatiani bila sababu, lakini pia kutaondoa kabisa uhuru wa habari nchini” iliongeza kusema

Post a Comment

أحدث أقدم